December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shahada nne za udaktari wa heshima kwa Samia kielelezo cha uwajibikaji

Na Penina Malundo, TimesMajira Online, Uturuki

JANA Rais Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari katika Uchumi na Chuo Kikuu cha Kikuu cha Ankara cha nchini Uturuki.

Uamuzi wa Rais Samia kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari ulifikiwa na Baraza la Chuo Kikuu cha Ankara, ambacho ni cha pili kwa ukubwa nchini Uturuki.

Baraza hilo, limeamua kwa kauli moja kumtunuku, Rais Samia Suluhu Hassan, Shahada ya Heshima ya Udaktari katika Uchumi kwa kutambua uongozi wake wa kipekee ambao umeleta mageuzi makubwa ya kijamii, kisiasa na kiuchumi nchini Tanzania.

Shahada ya Heshima ya Udaktari ambayo Rais Samia ametunikiwa na chuo hicho ni ya nne kutunukiwa Rais Samia katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake.

Mara ya kwanza aliiipa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Novemba 30, 2022, baadaye, Oktoba 10, 2023 alitunukiwa Shahada ya Heshima ya pili ya Udaktari wa Falsafa na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru.

Aidha, Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) kilimtunuku Shahada ya Heshima ya Usimamizi wa Utalii na Masoko. naKitendo cha Rais Samia kutunukiwa shahada hizo mfululizo katika kipindi cha miaka mitatu, sio tu kinamuingiza kwenye rekodi, bali kinadhihirisha jinsi vyuo hivyo vinavyotambua mchango wake.

Shahada ya Heshima ya Udaktari hutolewa kwa mtu ambaye ameonesha mafanikio katika eneo fulani, mafanikio hayo, ndiyo yanayozingatiwa zaidi katika kutoa shahada ya udaktari ya heshima.

Hatua hiyo inamaanisha chuo hicho na vyuo vingine vitatu vilivyotangulia, vinatambua mchango wake katika kile anachokifanya, kwamba kinafanana na mtu mwenye shahada hiyo.

Kwa uamuzi huo, hiyo ina maana kwamba vyuo hivyo vimetambua mchango wa Rais Samia kuwa ni mkubwa sana na unaonesha ni mtu mwenye umakini, weledi na welevu unaofanana na watu wenye shahada ya udaktari kwenye nchi husika.

***Kwa nini Chuo Kikuu cha Ankara kimemtunuku shahada hiyo?

Jibu la swali hilo, linajibiwa na uamuzi wa Baraza la Chuo Kikuu cha Ankara, ambalo linasema Uturuki, limeamua kwa kauli moja kumtunuku, Rais Samia, Shahada ya Heshima ya Udaktari katika Uchumi kwa kutambua uongozi wake wa kipekee ambao umeleta mageuzi makubwa ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi nchini.

Mageuzi yametajwa kuboresha ustawi wa Watanzania na kuimarisha sifa ya Tanzania ulimwenguni na yamekuza mahusiano ya kibiashara, kiuchumi na kisiasa kati ya Tanzania na nchi nyingine, ikiwemo Uturuki.

Hafla ya kukabidhiwa tuzo imeongozwa na Mkuu wa Chuo, Prof. Necdet Ünüvar na kushuhudiwa na Wahadhiri, wanafunzi wa Chuo hicho na mabalozi wa nchi za Afrika wanaowakilisha nchi zao Uturuki.

*** Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru

Aidha, Rais Rais Samia alitunukiwa udaktari wa heshima na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru (JNU) India kwa kutambua mchango wake katika kuchochea maendeleo ya watu nchini Tanzania.

Rais Samia alitunukiwa shahada hiyo Oktoba 10, 2023 . Akitangaza kumtunuku Rais Samia shahada hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru, Santishree Dhulipudi Pandit alisema Rais Samia ni mwanamke wa kwanza kuwa Rais nchini Tanzania.

Mwaka 1995, chuo hicho kilimtunuku Mwalimu Julius Nyerere udaktari wa heshima, hivyo, Rais Samia amekuwa kiongozi wa pili wa Tanzania kutunukiwa hehima hiyo na chuo hicho.

Akizungumza baada ya kutunukiwa shahada hiyo ya udaktari wa heshima, Rais Samia alikishukuru Chuo cha Jawahalal Nehru kwa kumtunukia shahada hiyo akieleza kwamba hiyo imeongeza kitu katika historia yake.

“Mmenibadilisha kama familia na kunitunuku shahada ya heshima (honoris causa), sasa nimesimama hapa kama mmoja wa familia ya Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru na siyo kama mgeni wa kawaida. Asanteni sana,” alisema Rais Samia.

Alikishukuru chuo hicho kwa kumpa heshima hiyo na kwamba anaikubali kwa kuwa anathamini uhusiano wa Tanzania na India na pia imeongeza kitu kwenye historia ya maisha yake.

“Shahada hii ya heshima itakuwa daima katika historia yangu kwa kuwa ya kwanza kutolewa kwangu na nchi ya kigeni. Ninayo moja kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lakini hii itakuwa ya kwanza kupewa na chuo cha nje,” alisema Rais Samia.

Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA)

Aidha, Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) kilimtunuku Rais Samia Shahada ya Udaktari wa Heshima ya Usimamizi wa Utalii na Masoko kwa sababu ya kuimarisha utalii wakati akiwa Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Utalii.

Akizungumza baada ais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi kumtunuku shahada hiyo, Desemba 28, 2023 mjini Unguja, katika mahafali ya 19 yaliyofanyika chuoni. Katika hotuba yake, Rais Samia bila kutaja siku, alisema alipopokea barua iliyoelezea nia ya yeye kutunukiwa shahada hiyo ilibidi awatafute baadhi ya watu aliofanya nao kazi alipokuwa Wizara ya Utalii na walimpa sababu za kukubali kutunukiwa shahada hiyo ikiwemo kuimarisha utalii.

Alieleza alipokuwa akihudumu katika wizara hiyo, alishirikiana na wenzake kuanzisha Baraza la Biashara Zanzibar ambalo kwa mara ya kwanza mwenyekiti alikuwa Rais Amani Abeid Karume na ndani ya miaka mitano walikuza biashara.

Pia alisema walimkumbusha jinsi alivyoimarisha uhusiano ya sekta ya umma na binafsi katika utalii, na alivyochochea uwekezaji wa hoteli zenye majina makubwa ikiwemo Kempiski, Zuri Residence aliyoipa kibali cha ujenzi.

Alisema akiwa wizara hiyo walitumia mwezi mmoja kuzunguka mabara tofauti duniani kuitangaza Zanzibar kama kituo kizuri cha utalii ikiwa ni ruhusa ya Rais Aman Abeid Karume. “Tulikwenda Uarabuni kuitangaza Zanzibar, Finland, Norway na Sweden kote kuisemea,” alisema.

Kuanzishwa kwa mchakato wa kurekebisha bustani ya Forodhani na kusimamia vizuri sekta ya utalii katika kipindi kigumu cha mdororo wa uchumi mwaka 2018 ni moja ya kitu kilichotajwa kuwa sababu ya kupewa shahada hiyo.

“Kipindi kile kuliibuka homa ya mafua, hivyo ilitulazimu kudhibiti taarifa za ugonjwa huo zisienee ili watalii waendelee kuja,” alisema.

Alitaja pia filamu ya Royal Tour aliyoifanya ikiwa ni mikakati ya kuitangaza nchi kupitia vivutio vya utalii vilivyopo. “Wakati tunafanya yote haya dhamira yetu ilisukumwa na kulenga kuwaletea maendeleo wananchi na kuimarisha ustawi wao, hatukuwaza kuwa ipo siku jitihada hizo zitaonekana na kupewa heshima hii,” alisema Samia.

Alisema shahada hiyo ni mahusus kwa Watanzania wote wanaompa moyo na ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yake akiwa mkuu wa nchi, watu wanaoifanya kazi katika sekta ya utalii na Rais mstaafu za Zanzibar, Abeid Aman Karume kutokana na malezi yake.

Alitumia nafasi hiyo kuwaasa wahitimu kutumia elimu zao kuleta mabadiliko chanya katika jamii, pindi wanaporudi majumbani na kuwataka kutambua wanapokwenda kuna changamoto nyingi za kimaisha, hivyo ni vyema kukabiliana nazo.

“Mawazo yenu yawe mema ukijiwazia mabaya moyo, mdomo kila kitu kitakuwa kinabeba mabaya,” alisema. Pia ameeleza kufurahishwa na wingi wa wanawake waliohitimu chuoni hapo ambao ni asilimia 58 ya wahitimu wote, huku akieleza hayo ni matokeo makubwa ya Serikali ya Zanzibar.

Alisema wakati akisoma, kadri darasa lilivyoongezeka ndiyo wasichana walipungua. “Hivyo hii asilimia 58 Serikali imefanya kazi kubwa, nawapongeza,” alisema Samia.

Kabla ya kumkaribisha Rais, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohammed Mussa amesema Rais Samia alistahili kupewa hadhi ya Profesa kutokana na uthubutu alioonyesha katika uongozi, ukomavu na uvumilivu wa kisiasa.

“Niliuliza wakati linakuja wazo la kupewa PHD kwani haiwezekani kupewa Profesa moja kwa moja? Wakasema kuna taratibu zake, lakini tutalishughulikia,” alisema Lela.

***Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)

Aidha, Rais Samia alitunukiwa shahada ya kwanza na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika mahafali ya 52 duru ya 5 yaliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam

Shahada hiyo ilidhihirisha na kusadifu kazi kubwa na zinazotekeleza na kiongozi huyo mkuu wa nchi.

Kazi kubwa na nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia ilikuwa chachu ya kutolewa kwa Shahada hiyo.

Uamuzi huo ni uthibitisho wa dhahiri wa kazi kubwa na nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia katika kuleta ustawi wa maisha na maendeleo endelevu kwa nchi.

Kazi kubwa iliyofanyika na kupelekea kutunukiwa shahada hiyo ni pamoja na mageuzi ya kiuchumi, kuimarisha misingi ya demokrasia, utawala bora na kuleta maendeleo ya jamii.

Rais Samia ameleta furaha na tumaini jipya miongoni mwa wananchi mambo yaliyochagizwa na utashi wake wa kisiasa, ukomavu na umahiri alionao katika uongozi.

Shahada hizo ni fahari inaonesha kuwa ni Rais anayewajibika kwa maslahi ya wote na zitampa moyo kuwa wananchi na dunia inaona kazi nzuri anazozifanya kwa taifa hivyo kumpa ari na nguvu ya kuendelea kutekeleza wajibu wake.