January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mshambuliaji wa mpya wa Simba Chris Mugalu (kulia), akifunga bao lake la kwanza katika Ligi Kuu Tanzania Bara

Shabiki anatafuta furaha wazee wa Simba wanalijua hilo

Na Philemon Muhanuzi, TimesMajira Online

KUNA mijadala inaendelea mitandaoni ambayo waanzishaji ni wanayanga wakiwazodoa wanasimba. Ujumbe wa wanayanga hao ni kwamba Simba imeuza timu na imeuza heshima kwa Mohamed Dewji kwa kukubali kubadilisha mfumo wa uendeshaji.

Hazipiti siku mbili pasipo wanayanga kurusha video au audio zenye kuhusu namna wazee wa Simba wasivyoyabariki mabadiliko yanayoendelea ndani ya klabu.

Wanayanga wanayo yao yenye haki ya kuwashughulisha lakini kiushabiki wanachokifanya ni jambo lenye kukubalika. Klabu yao haijabariki aina ya mabadiliko yatakayoonyesha muelekeo mpya. Bado yao ni klabu ya wanachama, wana sauti ya maamuzi.

Hivyo wanatumia vyombo vya habari katika kujaribu kuwakera wanasimba. Katika kujaribu kuwaambia kwamba kukubali kuingia kwenye mfumo mpya ni kuuza utu wao.

Zinarushwa mitandaoni audio zenye kueleza ni upungufu upi ambao unakwamisha michakato ya Simba kubadilika kutoka katika mfumo wa wanachama na kuingia katika mfumo wa wanahisa.

Lakini hakuna ambacho chini ya jua kinaweza kisifanikishwe ikiwa lengo ni moja la wenye kukaa pamoja na kufanya wayafanyayo kwa ushirikiano.

Hizo taratibu za kutoka kuwa timu ya wanachama na kuwa ni mali ya wanahisa kama zinayo makosa ni rahisi kufanyiwa kazi.

Makosa ya kisheria au kikanuni siku zote yanao utatuzi na hayawezi kuhalalisha timu kurudi katika maisha yale yale ya kutembeza bakuli.

Simba yenye kuyakumbatia mabadiliko inazo fursa nyingi za kuweza kujiendesha kisasa kulinganisha na ile ya wanachama. Timu ambayo ni mali ya wanachama na yenye kujiendesha kwa nguvu za wanachama inayo mipaka ya ukuaji wake.

Sidhani kama mwanasimba mwenye kuijua dunia ya kisasa yenye kupatikana kirahisi tu mitandaoni, anaweza kukubaliana na masuala ya timu kujiendea tu kiholela. Kuringia umiliki wa timu wakati haina uwezo wa kushindana kimataifa ni kujifariji tu.

Na vilabu hivi viwili vya kariakoo siku zote vina wingi wa wanachama wenye kupenda kujifariji. Lakini huwezi kushindana na vilabu bora afrika kwa kutegemea michango ya mpesa, tigopesa na airtel money.

Hakuna kitu kama hicho. Timu moja ya Tunisia au Misri inayo jeuri ya kumnunua mchezaji kutoka Asia, Ulaya na Afrika kwa dola milioni tano au juu ya kiasi hicho, ambazo ni sawa na bilioni kumi za kitanzania.

Mohamed Dewji anapigiwa kelele na wadau wa Simba alipe shilingi bilioni ishirini ili aweze kuwa mwanahisa mwenye kumiliki asilimia 49 za umiliki.

Ina maana wachezaji wanne tu wa vilabu vya Afrika ya Kaskazini wanayo thamani yenye kulingana na umiliki wa hisa wa asilimia 49 wa klabu mmoja ya Tanzania!.

Hao wanasimba wakishirikiana na wanayanga wenye kuona kama vile mfumo wa kisasa wa uendeshaji wa mpira unawaondolea haki ya asili ya umiliki wa vilabu na wavitazame vilabu bora na tajiri vya afrika vinafananaje.

Pesa inayomgombanisha Mo Dewji na baadhi ya wanasimba wenye heshima na ushawishi mbele ya jamii, kwa vilabu vikubwa vya afrika inatumika katika kununua wachezaji wawili au watatu!.

Halafu baadhi ya wanachama wa Simba na Yanga wanadanganyana mitandaoni kwamba mfumo wa kutembeza bakuli unaweza kuzifikisha mahali hizi klabu mbili kongwe.

Upungufu wowote unaojitokeza wakati Simba ikiwa katika zoezi la kubadilisha aina ya uendeshaji, unao utatuzi ulioshawahi kutumiwa na vilabu vingine vya mataifa mengine.

Hawa wanachama wakongwe wasiotaka kunyumbulika kimtazamo wakumbuke tu kwamba shabiki anatafuta furaha. Shabiki analipia kiingilio chake pale uwanja wa Taifa ili aipate furaha ya kuona soka la kitabuni lenye kwenda sambamba na magoli ya kuvutia.

Na starehe siku zote ina gharama kubwa. Muunganiko wa ufundishaji kati ya Sven Van Broeck na Suleiman Matola hauwezi kuwepo kama Simba haina uhakika wa pato kubwa ambalo linapatikana ndani ya mfumo wa kisasa wa uendeshaji wa timu.

Muunganiko wa Mugalu, Morrison, Miquessone, Bwalya na Chama haupatikani bure bure tu. Ufike wakati ambapo wanachama wakongwe wa Simba na Yanga wakatambua kuwa dunia ya sasa imeshabadilika, haifanani kabisa na ile ya wakati wa ujana wao.

Mashabiki wa kisasa wanaofuatilia mechi pale uwanjani huku mikononi wakifuatilia zile mechi za ligi kuu za Ulaya kwenye simu zao, wanatafuta furaha ya ushindi.

Kwamba wapo wanachama fulani wenye umri mkubwa wasiotaka kukubaliana na ukweli kwamba dunia imeshabadilika, kwa hao wa kizazi kipya ni habari isiyoweza kueleweka.

%%%%%%%%%%%%%%%