Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online – Dodoma
WAZIRI wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ametoa taswira ya mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC), hususan kupitia utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR).
Mafanikio haya si tu kwamba yameongeza ufanisi wa usafirishaji wa abiria na mizigo bali pia yamefungua ukurasa mpya wa ukuaji wa uchumi na ushirikiano wa kikanda.
Katika hotuba yake ya Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 iliyosomwa mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Prof.Mbarawa amesema kwa mara ya kwanza katika historia ya usafiri wa reli nchini, huduma ya treni ya SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma ilizinduliwa rasmi Agosti Mosi 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo tangu kuanza kwa huduma hiyo, abiria zaidi ya milioni 2 wamesafirishwa kwa ufanisi mkubwa, huku muda wa safari ukipunguzwa kutoka saa tisa hadi saa tatu pekee.
“Mafanikio ambayo yameleta tija katika shughuli za kiuchumi na kijamii.”amesisitiza
Mtandao wa Reli ya Kisasa Waenea kwa Kasi
i
Kwa mujibu wa Prof. Mbarawa, ujenzi wa reli ya SGR unatekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza yenye urefu wa kilomita 1,219 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza imefikia hatua za mwisho.
Aidha amesema ,kipande cha Dar es Salaam–Morogoro (km 300) kimefikia asilimia 99.72 huku kazi za kuunganisha njia hadi bandarini zikiendelea.
Pia amesema, kipande cha Morogoro–Makutupora (km 422) kimekamilika kwa zaidi ya asilimia 97, kikijumuisha stesheni, vivuko na mifumo ya umeme na mawasiliano.
Kwa mujibu wa Waziri huyo ,katika awamu ya pili, Serikali imeanza ujenzi wa vipande vya Tabora–Kigoma na Uvinza–Musongati (km 240), ambapo hatua hii inalenga kuunganisha Tanzania na Burundi, na kufungua fursa kubwa za kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
SGR Kuzindua Huduma ya Mizigo Juni 2025
Amesema,moja ya mafanikio yanayotarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ni kuanza kwa huduma ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli ya SGR kuanzia Juni 2025.
Aidha amesema,Serikali tayari inatekeleza mkakati wa kuunganisha mizigo kupitia Shoroba za Kiuchumi za Cold Chain (mazao ya kilimo na samaki), Yellow Chain (madini), na General Cargo Chain (mizigo ya viwandani).
“TRC pia inashirikiana na taasisi kama WFP na Central Corridor (CCTTFA) kuhakikisha kuwa mizigo mingi inahamia reli, kupunguza gharama na kuongeza ufanisi wa biashara.”amesema Prof.Mbarawa
Mitambo ya Kisasa Yaboresha Huduma
Katika kuhakikisha huduma za SGR zinakuwa bora na za kisasa amesema, Serikali imenunua vichwa 17 vya treni ya umeme, seti 10 za treni ya EMU kwa abiria, na mabehewa ya abiria 89, ambapo 71 tayari yamewasili na kwamba kwa upande wa mizigo, mabehewa 1,430 yanatengenezwa, huku 264 yakiwa tayari nchini.
TRC Yaendeleza Maboresho ya Reli ya Kale ya MGR
Kwa mujibu wa Prof.Mbarawa ,pamoja na maendeleo ya SGR, TRC inaendelea kuboresha reli ya zamani ya MGR ili iendelee kutoa huduma.
Amesema ,miradi ya ukarabati inaendelea katika maeneo kama Kaliua–Mpanda, Dar es Salaam–Isaka, na Tanga–Arusha. Vichwa vya treni na mabehewa zaidi ya 350 ya mizigo na 33 ya abiria vimekarabatiwa na kuanza kutoa huduma.
Hata hivyo amesema pamoja na m hay lakini pia zipo baadhi ya changamoto zinazoikabili shirika hilo ikiwa ni pamoja na uharibifu wa miundombinu ya reli hususan nyaya za mawasiliano na uzio wa usalama wa reli ya SGR akisisitiza kuwa serikali haitamvumilia yeyote anayehujumu maendeleo haya.
“Hii ni tunu ya Taifa, na hatua kali zinachukuliwa dhidi ya wote wanaojihusisha na uharibifu wa miundombinu,” alisema Waziri.
Amesema,mradi wa SGR si tu mradi wa miundombinu bali ni chombo cha kimkakati cha kuimarisha uchumi, kukuza biashara, na kuunganisha Tanzania na nchi jirani.
Kwa hatua zilizofikiwa na mikakati iliyowekwa, Shirika la Reli Tanzania limeonyesha kuwa ndoto ya kuwa na mfumo wa usafirishaji wa kisasa inawezekana – na iko mbioni kuwa mfano wa kuigwa Afrika.
More Stories
Doreen: ‘Msiwafiche watoto wenye utindio wa Ubongo
Serikali yawezesha miradi 80 kwa utaratibu wa PPP
Mpogolo akabidhi Cheti kwa wahitimu