January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Seth aachiwa,kuilipa Serikali fidia

Na Grace Gurisha, TimesMajira Online

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme (IPTL), Herbinder Seth kwa masharti ya kutokutenda makosa yoyote kwa kipindi cha mwaka mmoja na pia amekubali kulipa fidia ya sh.bilioni 26.9, baada ya kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Hukumu hiyo, imesomwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili kuhusiana na unafuu wa adhabu ya mshtakiwa (Seth).

Shaidi amesema, Mahakama imemkuta na hatia mshtakiwa baada ya kukiri kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ambao ni dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.

Amesema ni wazi kwamba, Wakili wa Serikali Mkuu, Martenus Marandu amebaini kuwa Seth ni mkosaji wa mara ya kwanza na pia amekubali kuingia makubaliano ya kumaliza kesi na DPP ili kufanya jambo hili liishe kwa njia mwafaka na Serikali ambayo haiumizi pande zote mbili.

Pia, ni wazi kwamba amekubali kulipa fedha nyingi kwa Serikali, kwa hiyo atatakiwa kuzingatia alichokubaliana na DPP cha kulipa fedha hiyo, kwa hiyo anatakiwa kupewa adhabu ambayo itamfanya alipe hicho kiasi.

“Ni dhahiri kwamba umekaa muda mrefu wa kutosha gerezani, takribani miaka minne ni muda mwingine wa kutosha sana kukaa kwako ndani umeona mengi na umejifunza mengi, kumepita maji mengi kwenye daraja lako.

“Mahakama inaamua, kwa kuzingatia yote yaliyodaiwa na pande zote mbili, usitende makosa tena na pia utakuwa chini ya uangalizi kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia leo,” amesema Hakimu Shaidi.

Aidha, Seth ameweka hati ya mtambo wa kufua umeme wa IPTL namba 45566 uliopo kiwanja namba 292/2 kilichopo Kunduchi Salasala kama dhamana iwapo atashindwa kulipa fedha hizo.

Hata hivyo, mshtakiwa Seth ameshalipa kiasi cha sh.milioni 200 na kiasi kilichobakia anatakiwa kukilipa ndani ya miezi 12, kuanzia Juni 16, 2021.