Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
SERIKALI pamoja na uongozi wa Jumuiya ya wafanyabiashara nchini waafikiana kusimamia maazimio 15 huku serikali ikitoa maagizo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Mamlaka zingine husika.
Akizungumza na waandishi habari jijini hapa leo Juni 27, 2024 Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali,Thobias Makoba ameeleza kuwa kumekuwa na majadiliano kwa ngazi mbalimbali Kati ya serikali na viongozi wa jumuiya ya wafanyabiashara hapa nchini.
Mazungumzo hayo yalitokana na madai na hoja takribani 41 ambazo wafanyabiashara waliziwasilisha serikalini ikiwa ni sehemu ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchi.
Kutokana na hayo Makoba amesema wamekuja na maazimio hayo 15 ambayo ni Maamlaka ya Mapato Tanzania TRA kusitisha Mara moja mazoezi yote ya kamata kamata pamoja na kusitisha mazoezi mengine yote ya ufuatiliaji wa risisti za EFD katika maeneo yote nchini hadi mwezi Agosti, 2024 pamoja kusitishwa huko wafanyabishara wanahimizwa kuelendelea kutoa risiti za mauzo.
Aidha TRA inaagizwa kuweka mfumo mzuri utakaowezesha utoaji wa nyaraka muhimu za manunuzi wakati wa uingizaji wa bidhaa nchini kuanzia Julai, 2024 ambapo utekelezaji wake utawekewa utaratibu mzuri kwa kushirikisha wadau wote muhimu.
Ameeleza Serikali inaiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania kuongeza haraka Bandari Kavu (ICD) kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa mizigo kupitia utaratibu wa de-consolidation.
Vilevile TRA imeelekezwa kuongeza nguvu kwenye kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kodi na maboresho ya kodi yanayofanyika ili kuwezesha kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara kuhusu masuala ya kodi nchini huku Taasisi husika za Serikali pamoja na mabaraza ya biashara yashirikishwe kikamilifu katika ngazi zote.
Pia TRA imeelekezwa kubainisha na kusimamia vyema orodha ya bidhaa nane ambazo zitawekewa bei elekezi kama ilivyo katika bidhaa za magari yaliyotumika ambapo bidhaa hizo ni vitenge, mashati, nguo nyingine, vipodozi, vito vya thamani, nguo za ndani, leso na vesti.
“Serikali kwa ujumla itaendelea na zoezi la kuwapanga na kuwawekea mazingira rafiki wafanyabiashara wadogo ambao hawako kwenye maeneo rasmi ili kurahisha usimamizi, ufuatiliaji na urasimishaji wao wa biashara,”amesema Makoba.
Makoba ameeleza kuwa katika kipindi cha muda wa kati, Serikali itaendelea kufanya mapitio ya viwango vya kodi tulivyo navyo kwa sasa ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipa kodi kwa amani na haki kulingana na thamani ya biashara zao.
Vilevile, Katika kipindi cha muda mfupi na wa kati, Serikali itashughulikia changamoto zote za wafanyabaishara zilizowasilishwa Serikalini hususan zile ambazo hazihitaji mabadiliko ya sera au sheria;
“Katika maboresho zaidi, Serikali inaigiza TRA ikamilishe maboresho ya mfumo wa TANCIS ambao utajumuisha moduli ya Auto valuation itakayoweka wazi na usawa katika ukokotoaji wa kodi kufikia Januari 2025.
“Wataalam wa TBS na TRA kwa pamoja wameelekezwa kukamilisha marekebisho ya mfumo wa TEHAMA ili mizigo inayoingia nchini kwa njia ya uchangiaji makasha iweze kugombolewa kwa namba ya usajili wa mlipakodi (TIN) ya mwenye mzigo badala ya TIN ya wakala bila ya kuwa na gharama za ziada kwa mlipakodi ambapo zoezi hili linatarajiwa kukamilika Julai, 2024,” amesema.
Vilevile Serikali imeelekeza Wizara ya Fedha kuratibu zoezi la kufanya uchambuzi, tathmini na mapitio ya mfumo mzima wa utozaji na ukusanyaji pamoja na viwango vya Ushuru wa Huduma (Service Levy) pamoja na kushauri njia mbadala ya utozaji itakayo kuwa rafiki zaidi kwa wafanyabiashara ili kulinda mitaji na ukuaji wa biashara nchini.
Akizungumzia Kuhusu wafanyabiashara kutoka nje ya nchi,Makoba amesema kuwa Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na mamlaka zingine husika itaendelea kuimarisha ukaguzi wa vibali vya kazi kwa wageni ili kuhakikisha kuwa wamiliki wa vibali hivyo wanafuata masharti ya vibali hivyo kwa mujibu wa Sheria za nchi.
“Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wanaokiuka Sheria, Kanuni, Taratibu na Masharti ya vibali vya ajira ikiwa ni pamoja na kuwafukuza nchini na waajiri husika kuchukuliwa hatua za kisheria, ” amesema.
Ameeleza kuwa Mawaziri wanaohusika na sekta ya biashara wakutane na wafanyabiashara wote nchini kwa ajili ya kusikiliza changamoto za wafanyabiashara pamoja na kupokea maoni yatakayolenga kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini wakati wote.
Ameeleza Wataalamu wa Forodha wakutane na Jumuiya ya Wafanyabishara nchini mara moja ili kujadiliana kuhusu taratibu za kiforodha hususani uthaminishaji na ugomboaji wa mizigo. Suala hili likamilike ifikapo tarehe 10 Julai, 2024.
Pia amesema Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) itaendelea kuratibu suala la kutoa mrejesho kwa wafanyabiashara kila robo mwaka kuhusu utekelezaji wa mazimio baina ya wafanyabiashara na Serikali.
Kutokana na maazimio hayo na maagizo ya Serikali, pande zote mbili zimekubakiana hali ya biashara kote nchini kuendelea kama kawaida ili kuwapa watanzania huduma wanazostahili.
“Kwa maslahi mapana ya nchi yetu, Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wote kama ambavyo Rais amekuwa akisisitiza katika uongozi wake,”amesema.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato