“Megawati 70 za umeme zimeshatengwa kwa ajili ya SGR hivyo hakuna cha kukwamisha mradi huo kwenye nishati hata kama ungeanza leo,”ameeleza Waziri Dkt. Kalemani.
Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
SERIKLI imesema kuwa,hali ya upatikanaji umeme kwa sasa nchini ni nzuri ambapo wana ziada ya kutosha kwani wanazalisha zaidi ya Megawati 1,604 wakati matumizi ya Watanzania ni Megawati 1,180 kwa sasa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani wakati wa semina iliyoandaliwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambayo imewakutanisha pamoja wahariri na waandishi waandamizi mkoani Morogoro kutoka vyombo mbalimbali vya habari.
Dkt. Kalemani amesema,kutokana na uzalishaji huo pamoja na matumizi ya Watanzania kwa sasa wana ziada ya zaidi ya Megawati 400, kiwango ambacho ni kikubwa.
Pia amesema, hali halisi kwenye mabwawa ya uzalishaji umeme ni nzuri katika mabwawa yote saba ya kuzalisha umeme huku akitolea mfano bwawa la Mtera ambalo limejaa na kufikia kikomo chake cha nita za ujazo 698.76.
Waziri Dkt. Kalemani amesema, wanatarajia kulifungulia bwawa hilo hivi karibuni, kupunguza maji kwa lengo la kuilinda miundombinu iliyopo na inayolizunguka.
Amesema,Bwawa la Kidatu nalo limejaa kufikia mita za ujazo 448.81 wakati uwezo wake ni mita za ujazo 450 huku akisema kwa upande wa Mradi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) unaendelea vizuri.
Dkt. Kalemani amesema kuwa, kazi zote tano muhimu za ujenzi zinaendelea vyema na mkandarasi ameshalipwa zaidi ya shilingi trilioni 1.9 sawa na zaidi ya asilimia 100 aliyotakiwa kulipwa.
Amesema, faida za mradi mbali na umeme wa uhakika, utasaidia kuokoa mazingira ikiwemo ukataji miti ambapo akitolea mfano jijini Dar es Salaam magunia ya mkaa kati ya 400,000 mpaka 500,000 yanatumika.
Amesema JNHPP mpaka sasa imeshazalisha ajira zaidi ya 7,000 za moja kwa moja na zisizizo za moja kwa moja huku mradi huo ukienda sambamba kufunga minara ambapo hadi sasa wameshafunga minara 456 ya umeme na kipande cha Dar es Salaam hadi Kingolwira kimekamilika na kinasubiriwa ni majaribio.
“Megawati 70 za umeme zimeshatengwa kwa ajili ya SGR hivyo hakuna cha kukwamisha mradi huo kwenye nishati hata kama ungeanza leo,”ameeleza Waziri Dkt. Kalemani.
Kuhusu usambazaji umeme vijiji kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Waziri Dkt. Kalemani amesema hadi sasa vijiji 10,263 vimeshapata umeme kati ya vijiji 12,268 ambapo hadi 2024 vitakuwa vimepata umeme.
Dkt.Kalemani amesema Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeimarika kutoka kuendeshwa kwa hasara ambapo lilikuwa linapokea ruzuku ya shilingi bilioni 438 kutoka serikalini, lakini tangu mwaka 2017,halipokei tena ruzuku.
“Shirika la Umeme nchini (TANESCO) limeondokana na hasara ya shilingi bilioni 478 toka mwaka 2017, kufuatia kuondokana na uendeshaji wa mashine za mafuta mazito na dharura, ikiwemo usitishaji wa mikataba na kampuni zikiwemo IPTL,”amefafanua Waziri Kalemani.
Wakati huo huo, Waziri Dkt. Kalemani amesema wameokoa hasara ya shilingi bilioni 720 kwa mwezi kufuatia kuondoa mashine za mafuta mazito na dharura katika mikoa 12 nchini.
Dkt.Kalemani amesema gesi asilia inazalisha asilimia 52 ya umeme wote unaotumika nchini.“Pamoja na kuzalisha umeme, gesi asilia sasa inaunganishwa kwa matumizi ya nyumbani ambapo mpaka sasa jumla ya nyumba 3,000 zimeunganishwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara pia magari 350 yameshaanza matumizi ya gesi asilia badala ya petroli na dizeli na kuokoa asilimia 45 ya matumizi ya bidhaa hizo za mafuta nchini,” amefafanua Waziri Dkt. Kalemani.
More Stories
Serikali kuwezesha CBE kuwa kituo mahiri
TCC yaibuka kidedea tuzo za PMAYA
Mwanafunzi apoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba