January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali,kuongeza uzalishaji mazao ya baharini

Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online,Tanga

Serikali Mkoa wa Tanga,imetangaza adhima ya kuongeza kiwango cha uzalishaji samaki na mazao ya baharini.Hatua itakayoendana na uimarishaji wa ulinzi na usalama wa rasilimali zilizopo kwenye sekta ya uvuvi mkoani humo.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, ameyasema hayo, Septemba 19,2024,kwenye kikao kilichoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa ajili ya kujadili masuala ya uhifadhi wa bahari kwa vizazi na maendeleo ya sekta hiyo mkoani Tanga.

Dkt.Batilda,amesema, uvuvi ni moja ya sekta muhimu mkoani Tanga, hususani kwenye Wilaya za Tanga, Pangani, Mkinga, na Muheza,ambapo takwimu zinaonesha kuwepo jumla ya wavuvi 13,336 na vyombo vya uvuvi vilivyosajiliwa 1,922.

Ambapo ametoa mfano kuwa, uzalishaji wa zao la mwani linalolimwa baharini na wakulima 5,300, umefikia tani 3,000 kwa thamani ya takribani bilioni 5, kiasi kinachotarajiwa kuongezeka kufikia tani tani 5,000.

Pia amesema katika kipindi cha 2023/2024, samaki waliouzwa mkoani humo walikuwa na thamani ya bilioni 47.208, zilizowezesha ukusanyaji ushuru uliofikia takribani milioni 951.7.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia uvuvi, Dkt.Edwin Mhede, amesema viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri, wanapaswa kuendeleza kwa ufanisi zaidi usimamizi wa rasilimali za baharini unaozihusisha jamii zinazoishi kuzunguka maeneo yao.

Amesema hatua hiyo ni kama inayofanywa na Balozi Dkt Batilda, anayemtaja kuwa ni ‘Champion’ wa ulinzi wa rasilimali za bahari na mazao yake, kutokana na jitihada mbalimbali anazozifanya katika sekta hiyo mkoani Tanga.

Kwa mujibu wa Dkt Mhede, sekta ya uvuvi ina wavuvi milioni 6 nchini, sawa na asilimia 10 ya Watanzania, inaweza kuchangia mageuzi makubwa ya kiuchumi kadri inavyoshirikishwa kwenye mipango ya uzalishaji na masoko.

Naye Mkurugenzi wa Uvuvi, Profesa Mohammed Sheikh ametoa wito kwa Sekretarieti za Mikoa kusimamia halmashauri kutekeleza sheria, kanuni na miongozo ya uvuvi.Kupitia sera, sheria na kanuni za uvuvi, kuandaa miongozo ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi na mazingira yake, kupanga na kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya uvuvi.

Profesa Sheikh amesema, usimamizi wa rasilimali za uvuvi unapasa kuzingatia uandikishwa vyombo na wavuvi, usafirishaji na biashara ya mazao ya uvuvi kufanyika kwa mujibu wa sheria na kanuni, udhibiti wa zana haramu za uvuvi, usimamizi wa maeneo maalumu yaliyotengwa, kuthibiti ubora na usalama wa mazao ya uvuvi, masoko na usimamizi wa mialo ya kupokelea samaki.