January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yazindua kamati ya utekelezaji miradi ya maendeleo kwa kutumia  vyanzo mbadala

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

SERIKALI imezindua Timu ya Kitaifa ya  Kitaifa ya kuwezesha ugharamiaji wa miradi ya maendeleo kwa kutumia njia mbadala ili kuwezesha miradi mingi kutekelezeka na kukamilika badala ya kutegemea njia zilizozoeleka katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Lawrance Mafuru kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo wakati wa uzinduzi wa Timu ya Kitaifa ya kuwezesha ugharamiaji wa miradi ya maendeleo kwa kutumia njia mbadala (APF).

“Serikali imekuwa ikitekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo kwa lengo la kukuza uchumi na kuondoa umasikini…,kupitia mipango hiyo, miradi mbalimbali ya maendeleo imekuwa ikitekelezwa kupitia Bajeti ya Serikali. Alisema na kuongeza kuwa

“Hata hivyo, ugharamiaji wa miradi kwa utaratibu huu umekuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti ya Serikali na hivyo miradi mingi kupata fedha kidogo na kutokamilika kwa wakati. “

Hata hivyo alisema, utaratibu huo umekuwa ukisababisha Serikali kutotekeleza miradi ya kijamii kwa wakati.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Lawrence Mafuru akipokea kwa niaba ya Serikali Hundi ya shilingi milioni 460.4kutoka kwa Mwakilishi Mkazi wa Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) Bw. Peter Malika, zitakazoiwezesha Timu ya Kitaifa iliyoundwa kwa ajili ya Kuwezesha Ugharamiaji wa Miradi ya Maendeleo kwa kutumia njia mbadala (Alternative Project Financing – APF National Facilitation Team) kutekeleza majukumu yake kikamilifu

Mafuru alisema,utekelezaji wa mradi huo ni  utakelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/21-2029/30 ambapo miongoni mwa malengo ya Mpango huo ni kuhakikisha upatikanaji wa fedha za muda mrefu kwa ajili ya kugharamia miradi ya kimkakati.

“AFP ni utaratibu wa kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kutumia njia mbadala nje ya utaratibu wa kawaida wa kutumia bajeti ya Serikali. “alisema

Alisema,utaratibu huo utaiwezesha Serikali kugharamia miradi mikubwa ya kimkakati na yenye uwezo wa kuzalisha mapato pasipo na kutumia vyanzo vyake vya mapato moja kwa moja.

Aidha alisema, utaratibu huo utaiwezesha Serikali kuwa na uwezo zaidi wa kugharamia miradi ya kijamii ambayo haina sura ya kibiashara na hasa ile inayogusa jamii.

“ Hii inatokana na ukweli kwamba mahitaji ya ugharamiaji wa miradi ya Serikali ni makubwa ukilinganisha na mapato yanayotokana na vyanzo vyake.”alisisitiza

Akitolea mfano utekelezaji wa mipango ya serikali iliyotangulia,Mafuru alisema ,utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP II) ulitarajiwa kugharamiwa kwa kiasi cha Shilingi trilioni 107, hata hivyo malengo hayo hayakuweza kufikiwa.

Aidha alisema  utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP III) utagharimu kiasi cha Shilingi trilioni 114.9 ikijumuisha Shilingi trilioni 74.3 kutoka sekta ya umma na shilingi trilioni 40.6 kutoka sekta binafsi.

“Hivyo, ni wazi kuwa utaratibu huu ni muhimu sana katika kipindi hiki ambacho Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.”alisema

Kwa mujibu waMafuru, utaratibu huo utaiwezesha nchi kufikia baadhi ya malengo ikiwa ni pamoja na kupunguza presha kwenye Bajeti ya Serikali katika kugharamia miradi,kupata mchango wa sekta binafsi katika kugharamia miradi ya kimkakati,kuharakisha utekelezaji wa miradi na kuongezeka kwa utendaji na ufanisi wa utekelezaji wa miradi.

Alisema,pampoja na mambo mengine timu hiyo itakuwa na  jukumu la kujengea uwezo Wizara, Idara, Taasisi, Wakala na Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kuandaa maandiko ya miradi na kufanya upembuzi yakinifu pamoja na kuratibu uandaaji wa maandiko ya Miradi itakayogharamiwa kwa njia mbadala na kuratibu utoaji wa elimu kwa umma.

Baadhi ya wajumbe wa Timu ya Kitaifa ya Kuwezesha Ugharamiaji wa Miradi ya Maendeleo kwa kutumia njia mbadala wakionesha vitendea kazi walivyokabidhiwa baada ya kuzinduliwa kwa timu hiyo katika tukio lililofanyika Wizara ya Fedha na Mipango katika ukumbi wa Kambarage, Jijini Dodoma.

Ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa Timu hiyo kutekeleza  majukumu yake kwa weledi na uadilifu wa hali ya juu kwa manufaa ya Taifa huku akiwataka wadau wote wa sekta ya fedha kuendelea kutoa ufadhili wa utekelezaji wa jambo hili.

Vile vile ametoa wito kwa Taasisi za Umma zote zenye miradi inayokidhi vigezo vya APF kutumia njia hiyo mbadala ya miradi yote kupelekwa kama ilivyozoeleka Kupitia bajeti ya Serikali.

Akizungumzia mradi huo Kamishana wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Charles Mwamwaja alisema, Serikali inahitaji kufanya miradi mingi hivyo lazima na sekta binafsi ishiriki ili kufikia azma hiyo.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Mfuko wa Maendeleo na Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) Peter Malika amesema,shirika hilo limetoa ruzuku ya shilingi milioni 460 ili kuiwezesha  Timu hiyo ya Kitaifa kuandaa miradi kupitia vyanzo mbadala vya fedha kama ilivyokusudiwa.