December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yazidi kuweka mazingira mazuri kwa wajasiliamari wanawake

Na Mwandishi wetu, timesmajira

KUTOKANA na Serikali kuweka mazingira wezeshi ya biashara kwa wanawake nchini,bado wanawake nchini wametakiwa kuungana kwa pamoja kwa lengo la kutumia fursa mbalimbali zilizopo ndani na nje ya nchi ili kuweza kujikwamua kiuchumi.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) Mercy Sila wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la chama hicho lililopo kwenye maonesho ya 47 ya biashara ya Kimataifa yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere.

Amesema kwa sasa fursa za kiuchumi ni nyingi tofauti na miaka ya nyuma kwani Serikali imekwisha weka mazingira wezeshi kwa kundi la wanawake wajasiriamali .

“Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wajasiriamali kuweza kufanyabiashara bila usumbufu wa aina yoyote, tumeona kwenye bajeti ya mwaka huu vitu vingi vimerekebishwa ili kumuwezesha huyu mama mwenye kipato cha chini kuweza kufanya biashara na kupata faida,” amesema Sila

Amesema Chama chao kina jukumu kubwa ni kuwaunganisha wanawake wafanyabiashara na wajasiriamali Tanzania nzima kwa kuwaelewesha na kuwajulisha fursa mbalimbali zilizopo ili waweze kuzitumia hatimaye wajikwamue kiuchumi.

Kwa Upande wake Mratibu wa Shirika la Watu wa Kipato cha chini wanaoishi kwenye Makazi yasiyobimwa, Husna Shechonge amesema wamefika katika banda la TWCC ili kuweza kuangalia wanawake wenzao namna wanavyofanya shughuli zao za kijasiriamali na mafanikio yao kiujumla.

“Tumefanya ziara ya kuja kuona ni namna gani wanawake wa TWCC wanavyofanya shughuli zao za kibiashara,kupitia shirikisho letu tunaibua kero mbalimbali za wanawake na miradi mbalimbali ya ujasiriamali ambayo itatoa fursa kwa kundi hili kujikwamua kiuchumi lakini wanawake wanakwenda kujifunza kwa wenzao waliofanikiwa,” amesema.

Amesema shirikisho hilo lina jumla ya vikundi 814 vyenye wanachama wasiopungua 26,000 kwa Tanzania nzima na kwamba asilimia 80 ya wananchi wao ni wanawake na wananishughulisha katika masuala ya kuweka akiba na kukopeshana kwa lengo la kuondokana na umasikini.