January 29, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yazidi kuwakosha wawekezaji wadau waipa tano

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Dar

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepogezwa kwa kuweka mazingira bora na wezeshi kwa wawekezaji nchini, hivyo kuwezesha kulipa kodi kwa Serikali na kuchochea maeneeleo.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah baada ya kampuni hiyo kuibuka kinara kwa kupokea tuzo nne za mlipakodi bora wa mwaka zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Rais Dkt. Samia alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

“Mazingira mazuri na wezeshi yaliyowekwa na serikali chini ya uongozi wa Dk. Samia ndiyo yametuwezesha wawekezaji kufanya shughuli zetu katika mazingira mazuri, ndiyo maana sisi Puma Energy Tanzania tumapata tuzo zote.

“Tumekuwa walipakodi wazuri hususan katika sekta ya mafuta na gesi, ndiyo sababu ya kupata tuzo zote hizo. Kwa hiyo tunamshukuru Mungu lakini tunamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuweka mazingira yaliyo bora kwa wawekezaji kuendelea kufanya vizuri nchini,” amesema.

Fatma alisema kuwa wanaona zikopelekwa fedha zinazotokana kodi zinazolipwa na hatimae kuchochea maendeleo makubwa yanayoletwa nchini chi ya Rais Dk. Samia.

“Tumeona miradi mikubwa iliyozinduliwa mwaka 2024 lakini kuna miradi mingine mingi ambayo bado iko katika mchakato wa kuzinduliwa, kwa hiyo tunapolipa kodi tunajua fedha zetu zinakwenda wapi,” alieleza.

Aidha, aliongeza kuwa, tuzo zote ambazo Puma Energy Tanzania imezipata kutoka TRA zinatokana na uwajibikaji wao katika kulipa kodi kwa wakati na kwamba tuzo hizo ni chachu ya maandalizi ya mwaka ujao wa fedha kufanya vizuri zaidi.

Kupitia hafla hiyo Puma Energy Tanzania imetunukiwa tuzo ya mlipakodi anayekidhi viwango vya ubora katika ngazi ya kitaifa kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Pia kampuni hiyo kupitia kitengo chake cha Wet Cargo, imepata tuzo ya kutambua malipo ya wakati ya kampuni hiyo ya kodi na ushuru katika mwaka wa fedha 2023/2024 katika forodha na ushuru wakati wa siku ya mlipakodi nchini mwaka 2024.

Tuzo nyingine iliyopata Kampuni ya Puma Energy Tanzania Limited ni ya mshindi wa jumla katika kutambua ulipaji wa kodi na ushuru zilizolipwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 katika forodha na ushuru wakati wa siku ya kuthamini walipakodi mwaka 2024.

Kwa upande wa tuzo ya nne imetolewa kwa kampuni hiyo kupitia kitengo cha uagizaji wa Wet Cargo kutambua ushuru na ushuru mkubwa wa kampuni uliolipwa katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 katika forodha na ushuru 2024.

Tuzo za mlipa kodi Bora wa mwaka hutolewa kila mwaka na TRA ambapo taasisi hiyo hutoa zawadi kwa wafanyabiashara wanaolipa kodi katika makundi mbalimbali.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Rais Samia, amewataka Walipakodi nchini kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kuacha vitendo vya ukwepaji kodi ambavyo vinaondoa usawa wa ushindani sokoni.

Alisema utolewaji wa tuzo hizo unachochea ulipaji wa kodi kwa hiari na kuwataka wenye tabia za kukwepa kodi kuacha mara moja, kwani wanadhoofisha uchumi wa nchi na kuwavunja moyo Walipakodi waaminifu kwa kuweka ushindani usiokuwa sawa sokoni.

Rais Samia aliiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao ndiyo waliandaa tuzo hizo kuendelea kupambana na watu wanaokwepa Kodi kwa kuwasaka wanaoghushi risiti za EFD na VFD pamoja na wanaotumia Stempu bandia kwenye vinywaji.

“Dhuruma siyo kitu kizuri hivyo wanaokwepa Kodi watambue kuwa wanafanya dhuruma, hali kadhalika watumishi wa TRA wanaofanya makadirio yasiyokuwa sahihi nao wanafanya dhuruma, tuache,”alisema Dkt. Samia.

Dkt. Samia alisema mwelekeo wa Serikali ni kuongeza idadi ya walipakodi na siyo kuwatumia wachache waliopo na Hali hii itafanikishwa na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iwe rasmi na kulipa kodi kikamilifu.

Rais Samia alisema Ilani ya Uchaguzi ya CCM inaitaka nchi ipunguze utegemezi na utegemezi na utapungua kwa kusimamia kwa usahihi ukusanyaji wa kodi jambo ambalo litaifanya Tanzania ijiamini.

Rais Samia alisema Bajeti ya Serikali ni sh. Trilion 49.34 na miongoni mwa fedha hizo sh. Trilion 30.4 sawa na asilimia 61.6 inatokana na makusanyo ya kodi kutoka kwa TRA, hiyo ndiyo inaonesha tunavyoenda kujitegemea.

Alisema mwaka ujao 2025/2026 hakutakuwa na Tuzo za Mlipakodi za TRA bali kutakuwa na Tuzo za Rais ili kuonesha umuhimu wa kulipa Kodi.

“Kwenye masuala ya Kodi hakuna mzaha, mtu asijifanye kwamba ana maelekezo kutoka juu asilipe kodi, napenda kuwaambia hakuna mtu yoyote niliyemruhusu asilipe kodi na mimi ndiyo ngazi ya juu ya mwisho, kama nitamruhusu mtu yoyote nitatoa maagizo kwa barua,”alisisitiza Rais Samia

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda alisema siku ya shukrani kwa Mlipakodi ni maalum kwa ajili ya kuwatambua na kuwashukuru Walipakodi wote wakubwa na wadogo.

Alisema utoaji wa tuzo ni kutambua Walipakodi waliofanya vizuri katika sekta mbalimbali zikiwemo sekta ya Madini, Taasisi za Umma, Taasisi za Fedha, Sekta ya uzalishaji na Viwanda, Sekta ya Utalii, Walipakodi wakubwa na Tuzo ya Kamishna Mkuu.

Kamishna Mkuu Mwenda alivitaja vigezo vitano vilivyotumika kuwapata washindi wa tuzo kuwa ni Mlipakodi mwenye rekodi nzuri katika ulipaji wa Kodi, Mlipakodi anayelipa kwa hiari na kwa wakati, Mlipakodi anayetumia EFD mashine na VFD kikamilifu, Mlipakodi aliyelipa kodi kubwa zaidi na Mlipakodi anayetoa ushirikiano kwa TRA.

Alisema wapo washindi waliofanikisha makusanyo makubwa ya Kodi katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo TRA ilivuka malengo kwa kukusanya Sh. Trilion 16.528 ambao pia watatunukiwa.

“Mimi na wenzangu ndani ya TRA Tutaendelea kutekeleza maagizo yako yote, Tutaendelea kupambana na wanaofanya magendo, Tutaendelea kukusanya Kodi kwa kiwango kikubwa bila kuwa na migongano na Walipakodi, Tutaendelea kutatua migogoro na kuwasikiliza Walipakodi, Tutaendelea kutoa huduma Bora” alisema Kamishna Mkuu Mwenda