Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bi. Zuhura Yunus, ametoa wito kwa wakulima na wasindikaji wadogo wa zao la zabibu kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya kwa kueneza elimu na ujuzi walioupata ili kuongeza thamani ya mazao katika mnyororo wa kilimo.
Akizungumza leo 21 Oktoba, 2025 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kukuza ujuzi kwa wakulima na wasindikaji wadogo, Bi. Zuhura alisema mafunzo hayo yanawalenga wakulima takribani 1,000 nchini, yakiwa na lengo la kuboresha uzalishaji, kuongeza tija na ubora wa bidhaa, pamoja na utoaji wa huduma bora katika sekta ya kilimo.
“Lengo kuu la mafunzo haya ni kuongeza ufanisi katika uzalishaji, kuimarisha mbinu za utendaji kazi na kuboresha bidhaa, ili sekta ya kilimo iweze kuchangia kikamilifu katika uchumi wa nchi,” amesisitiza Bi. Zuhura.

Ameongeza kuwa wakulima na wazalishaji wadogo ni mhimili muhimu katika uzalishaji wa chakula na usambazaji wa malighafi kwa viwanda, lakini wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya ukosefu wa ujuzi wa mnyororo wa thamani. Hivyo, mafunzo haya yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo ili kuwawezesha kupata ujuzi unaohitajika.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Bi. Mary Uguzi ameishukuru Serikali kwa kutoa mafunzo yenye tija, huku akisema elimu hiyo itawasaidia kuongeza ubora wa bidhaa na ushindani sokoni. Naye Bw. Noha Madeje alisema wamejifunza mbinu bora za usindikaji wa zabibu hususan utengenezaji wa wine, na akaomba Serikali iendelee kuwawezesha kwa mikopo ili kuimarisha shughuli zao za kilimo na usindikaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dkt. Thomas Bwana, ambaye anaongoza timu ya wataalamu wanaotoa mafunzo hayo, aliwataka wakulima kutumia ujuzi walioupata kuwasaidia wenzao vijijini ili kuhakikisha mafanikio ya mafunzo yanaenea kwa upana zaidi.

“TARI tumejipanga kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti zetu yanamfikia mkulima na kuongeza tija. Mafanikio ya sekta ya kilimo yanatokana na matumizi ya maarifa sahihi,” amesema Dkt. Bwana.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Bi. Alana Nchimbi, ameeleza kuwa mafunzo haya yatafanyika katika mikoa minne kwa kuzingatia mazao yanayolimwa katika maeneo husika. Mikoa hiyo ni: Dodoma (zabibu), Singida (alizeti), Iringa (nyanya na mchicha lishe), na Mbeya (maharage na parachichi), ambapo wakulima 250 kutoka kila mkoa watanufaika.
Alana alifafanua kuwa mafunzo hayo yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni jitihada za kuimarisha nguvu kazi ya Taifa kwa kuipatia maarifa stahiki

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina