May 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yawezesha miradi 80 kwa utaratibu wa PPP

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

SERIKALI imewezesha miradi 80 ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kwa utaratibu wa Ubia kati ya Sekta za Umma na Sekta Binafsi (PPP).

Akizungumza bungeni jijini Dodoma mapema wiki hii, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza, aliyetaka kujua idadi ya miradi ambayo imewezesha na Serikali kwa utaratibu wa PPP.

Waziri Chande alisema, miradi mitatu kati ya hiyo tayari ipo katika hatua ya utekelezaji, minne ikiwa katika hatua ya majadiliano, miwili katika hatua ya ununuzi, 26 katika hatua ya upembuzi yakinifu, 13 ikiwa katika hatua ya upembuzi yakinifu wa awali huku miradi 32 ikiwa katika hatua ya andiko dhana.

“Sheria ya Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), imeanzisha mfuko wa uwezeshaji Ubia Yani PPP Facilitation Fund-PPPFF, kwa lengo la kuwezesha Mamlaka za Serikali kuandaa na kutekeleza miradi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi”, amesema Chande.

Ameeleza kuwa, sheria hiyo imekipa Kituo cha Ubia ( PPP Center) jukumu la kutoka usaidizi wa kiufundi kwa Mamlaka za Serikali na Sekta Binafsi wakati wa uibuaji, maandalizi, utekelezaji wa miradi ya Ubia kati ya Sekta za Umma na Sekta Binafsi.

Aidha akizungumzia ujenzi wa barabara ya Igawa- Tunduma kwa utaratibu wa PPP, Chande amesema, kwa Sasa yupo mshiriki kutoka Sekta Binafsi ambaye anaandaa mradi huo kupitia utaratibu wa PPP.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Tanzania na Zambia zipo kwenye majadiliano na Serikali ya China, akidai kuwa hadi sasa muelekeo ni mzuri na wakati wowote Serikali hizo zitatiliana Saini makubaliano kupitia kampuni ya China ya CECC kuhusu utekelezaji wa mradi huo.

Pia amesema Serikali unaendeleaje kuhamasisha sekta binafsi kushirikishwa kwenye hatua za uandaaji miradi ili wawe na mchango katika maendeleo ya nchi.