January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto 695,508 kupata chanjo ya polio Dodoma

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MRATIBU wa chanjo mkoa wa Dodoma Dkt.Francis Bujiku amesema,mkoa huo umepanga kuwafikia watoto wenye umri chini ya miaka mitano wapatao 695,508 kwa ajili ya kuwapa chanjo ya matone ya polio awamu ya nne .

Utoaji wa chanjo ya polio awamu ya nne umeanza Desemba Mosi mwaka huu na unatarajia kukamilika Desemba 4 mwaka huu huku akisema katika kampeni ya awamu ya tatu ya polio mkoa wa Dodoma ulilenga kuwafikia watoto 591,624 lakini ulivuka lengo kwa kuchanja watoto watoto 695,508.

Afya bora kwa mtoto ni moja ya afua muhimu zinazopaswa zitekelezwe kwa lengo la kuleta matokeo chanya katika ukuaji na maendeleo ya wali ya mtoto na kufikia maono.

Akizungumza na mtandao huu Dkt.Bujiku amesema,katika awamu ya tatu ya chanjo ya polio walivuka lengo kwa asilimia 117.6 huku akisema idadi ya watoto waliofikiwa ndiyo likawa lengo la kampeni ya chanjo awamu ya nne.

“Katika kampeni ya polio awamu ya tatu tuliweka lengo la kuwafikia watoto 591,624 lakini watoto waliochanja ni 695,508 sawa na asilimia 117.6 ya lengo tulilojiwekea .”amesema Bujiku

Aidha akizungumza wakati wa semina elekezi kwa waandishi wa habari kuhusu mipango ya serikali katika kukabiliana na ugonjwa wa polio Afisa Programu wa Chanjo Wizara ya Afya Lotalis Gadau amesema,serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na Ugonjwa wa polio kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano kwani ni miongoni mwa magonjwa hatarishi kwa kundi la watoto wenye umri huo.

“Ugonjwa huu huweza kuwasababishia watoto kupooza kifo kutokana na virus vya ugonjwa huo kuvamia mfumo wa neva na hivyo kuathiri malezi na makuzi yao na hivyo kushindwa kufikia utimilifu wao.

Aidha amesema,kama ilivyokuwa kwa chanjo zilizotangulia,chanjo hii pia itakuwa ni ya nyumba kwa nyumba kwa lengo la kuhakikisha watoto wote wa umri huo wanafikiwa.

Ametaja njia za maambukizi ya ugonjwa huo sambamba na dalili ikiwa ni pamoja na homa, uchovu, maumivu, ya kichwa, kutapika, kukakamaa shingo na maumivu ya Viungo.

Ugonjwa huu huambukizwa kwa kuingia mwilini kwa njia ya mdomo, kunywa Maji,au chakula ambacho kimechafuliwa na kinyesi kutoka kwa mtu aliyeambukizwa virusi hivyo na virusi huongezeka ndani ya utumbo na hutolewa na mtu aliyeambukizwa kwenye kinyesi, ambacho kinaweza kupitisha virusi kwa wengine

Hamida Ramadhani mkazi wa Maili mbili Jijini hapa ameiasa Serikali kuweka mikakati ya kujiridhisha kwamba watoa huduma hiyo ya chanjo kweli wanapita nyumba kwa nyumba kwa mujibu wa kampeni hiyo ili kuwafikia watoto wote.

“Nimesema hivi kwa sababu ninao uhakika kwamba watoa huduma hawapiti nyumba kwa nyumba kama inavyodaiwa na hivyo kusababisha baadhi ya watoto kutofikiwa na huduma hiyo ambayo huweza kusababisha madhara na kuathiri ukuaji wao,kwa hiyo ninaiomba serikali kutafuta namna ya kujiridhisha kwamba watoto wanapitiwa nyumba kwa nyumba.

Aidha ameeleza hali ilivyo kwa sasa juu ya ugonjwa wa Polio katika maeneo mbalimbali ndani ya Bara la Afrika.

Zambia tayari kuna kisa kimoja, wenyewe wanajiandaa na awamu ya Tatu, na kwetu Tanzania tunamshukuru mungu bado kisa ni kile kile hatujapata kingine, lakini bado hakijalemaa, bado tunaendelea na ufuatiliaji kwa kuchukua Sampuli kuhakikisha kwamba tunapeleka maabara mwisho wa siku watoto wetu wawe salama.DRC CONGO bado kuna vimlipuko vya hapa na pale lakini ambao tulienda nao sambamba tokea tunaanza mwanzo ni Malawi, Msumbiji, Zimababwe na Zambia

Pia ameeleza mikakati inayotumika katika kuhakikisha wanatokomeza ugonjwa huo hapa nchini ikiwa ni pamoja na kufanya kampeni za kutoa elimu itakayoambatana na utoaji wa Chanjo.

Tunachojitahidi ni kuonesha kwamba tunaimarisha utoaji wa chanjo za kila siku kuhakikisha kwamba watoto wetu wanakamilisha Ratiba zao za chanjo ili endapo hata Kirusi kikija kikimkuta mtoto ameshapata kinga kamili kinakuwa hakina nafasi na kwa awamu hii tunalenga kuwafikia watoto wapatao Millioni 14 laki sita na Tisini, Mia tano Tisini na Saba kwa awamu hii ya nne

Awali akifunga mafunzo hayo Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Dodoma  Dkt. Francis Bujiku amewataka wananchi kutoa ushirikiano pindi wanapowaona watoa huduma kwa kuwatoa watoto ili wapate Chanjo ya Polio ya matone ili  kuongeza kinga dhidi ya ugonjwa wa Polia ambao ni mkali na una madhara kwa watoto .