December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yawatoa hofu wawekezaji

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Waziri ya Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki amewatoa hofu wawekezaji na wafanyabiashara juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki akipokea maelezo kuhusu kiwanda cha uzalishaji wa vinywaji bariki ikiwemo maji, juisi na soda aina ya Asante kutoka kwa Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Katrini Mwimbe alipofanya ziara kiwandani hapo juzi. Kiwanda hicho kipo eneo la Chinyoya Dodoma.

Akizungumza mwishoni mwa wiki Jijini Dodoma, wakati wa ziara yake  ya kukagua shughuli za uzalishaji katika viwanda vinavyozalisha mvivyo kikiwemo Domiya Estate kinachozalisha vinywaji vikali na baridi kama soda, maji na chai baridi aina ya Asante na kiwanda  cha Alko Vintages Co. Ltd, Amesema kuwa Serikali ina mipango na mikakati ya kuhakikisha kuna mazingira bora ya uwekezaji.

“Serikali inatambua changamoto mnazopitia na imeweka mikakati ya kuhakikisha inazitatua ikiwemo uanzishwaji wa sheria mpya ya uwekezaji nchini inayolenga kuweka mazingira bora ya uwekezaji,”Amesema Waziri Kairuki

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki atoa majumuisho ya ziara yake katika eneo la uzalishaji la Domiyo Estate lililotengwa kwa ajili ya kuzalisha mvinyo, vyumba vya kulaza wageni, kiwanda cha vinywaji baridi mara baada ya ziara ya kukagua shughuli zinaoendelea katika eneo hilo wakati wa ziara yake Kijiji cha Chinyoya Dodoma.

Amesema, changamoto ambazo wawekezaji wamekuwa wakikabiliana nazo zinaendelea kutatuliwa ikiwa ni pamoja na utitiri wa kodi, ukosefu wa maji ya uhakika, ubovu wa miundombinu ya barabara, gharamza kubwa za uzalishaji, uzalishaji duni kwa ubora na wingi wa zabibu, ukosefu wa aina mabalimbali za zabibu.

Changamoto nyingine walizobainisha ni ugumu wa kuanzisha viwand vidogo vya kusindika zabibu, ukosefu wa utaalamu katika kilimo cha zabibu, pamoja na uwepo wa bidhaa zisizo na ubora sokoni.

Meneja Mkuu wa eneo la uzalishaji la DOMIYO ESTATE Katrini Mwimbe akimuonesha mazingira ya eneo hilo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki alipotembelea kukagua uzalishaji wa vinywaji vikali na baridi vinavyozalishwa kiwandani hapo.

Akijibu changamoto hizo, Waziri Kairuki aliwatoa hofu kwa kuainisha maeneo muhimu yaliyofanyiwa maboresho ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa tozo na kodi zaidi ya 168 nchini, kuendelea kuboresha miundombinu muhimu ikiwemo barabara zinazosimamiwa na TARURA,  kuwa na uhakika wa upatikanaji wa umeme na maji ili kila mwekezaji na mfanyabiashara anufaike na kuwekezaji kwake.

Aidha Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji kwa kushirikiana na Kituo  cha Uwekezaji nchini  inaendelea kuandaa mpango wa kuteua mabalozi kwa lengo la kuvutia wawekezaji kama ilivyo  katika sekta nyingine ikiwemo utalii.

“Tumeendelea na hatua za awali za kuanzishwa kwa mpango wa kuwa na mabalozi watakao tangaza masuala ya uwekezaji nchini, hii ni pamoja na kushirikisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kuona namna ya kupata mabalozi hao watakaofikia taifa na nje ya nchi,”amesisitiza Waziri Kairuki

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki akipokea maelezo ya vifaa vilivyomo katika vyumba vya kulala wageni katika hoteli ya DOMIYA kutoka kwa Meneja Mkuu wa hoteli hiyo alipofanya ziara yake ya kikazi.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwashauri wawekezaji kuvitumia vyema vyombo vya habari katika kutoa elimu na kujitangaza ili kuendelea kuwa na soko la uhakika kwa kuzingatia ubora wa bidhaa wanazozalisha.

Naye Mchumi Mkuu kutoka idara ya Uwekezaji, Francis Mollay, alibainisha baadhi ya jitihada za kuhakikisha wawekezaji wananufaika na uwekezaji wao pamoja na uwepo wa sheria na kanuni zinazobainisha namna bora ya kuboresha mazingira yao ili kuwa na maendeleo katika sekta zote.

“Tunaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kupitia sheria na sera zinazohusiana na kodi mbalimbali ili kutatua changamoto za kikodi zilizopo,”alifafanua Mollay.

Kwa upande wake mmiliki wa kiwanda cha kutengeneza mvinyo cha Alko Vintages, Archard Kato alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuendelea kuboresha mazingira ya wawekezaji na kutoa rai kwa vijana kutumia fursa zilizopo katika kilimo hasa cha zabibu kwa kuonesha nia na uthubuti ili kujikwamua kiuchumi na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki akioneshwa na kupewa maelezo kuhusu mtambo wa kuzalisha mvinyo kutoka kwa Mhandisi wa Kemikali na Mchakato tija wa kiwanda hicho, Daniel Mollel wakati wa ziara yake katika kiwanda cha kuzalisha mvinyo cha DOMIYA.

“Vijana lazima mjiamini na kuwa na uthubutu katika kuanzisha biashara ili kuingia kwenye sekta ya uwekezaji, hakikisha una maono au jambo linalokuvutia na weka mikakati ya kulifikia.Hakikisha unajaribu wazo ulilonalo na kuwatumia walioweza katika hilo, utayaona manufaa kama kijana,”Amesema Kato.

Kiwanda kingine alichotembelea ni Alko Vintages Co. Ltd kinachozalisha mvinyo wa aina mbalimbali ikiwemo Dompo, Altar, St. Mary’s, Image, Rose na Klymax viliyopo katika Wilaya ya Dodoma Mjini mkoani Dodoma.