November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yawatoa hofu wananchi wanaotumia usafiri wa vivuko Kigamboni

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

SERIKALI imewatoa hofu Wananchi wa mkoa wa Dar es salaam wanaotumia usafiri wa vivuko eneo la Kigamboni -Magogoni juu ya taharuki kuhusu huduma inayotolewa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) nakueleza kuwa imetengenezwa na watu wenye maslahi binafsi.

Hofu hiyo imetoa jiji hapa leo Mei 28,2024 na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wakati alipokuwa akifanya mahojiano na moja ya chombo cha habari cha televisheni hapa nchini ambapo amesema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha inaimarisha huduma ya usafiri wa vivuko nchini.

“Niwatoe wasiwasi Wananchi wa Dar es salaam pamoja na kigamboni, taharuki ambayo imetengenezwa hakukuwa na sababu ya kutengenezwa,lakini sisi tunaofahamu yapo maslahi binafsi nyuma ya utengenezaji wa hii taharuki,”amesema Bashungwa

Ameeleza kuwa sasa vivuko vingi vinaendelea na matengenezo, lakini pia Mkandarasi ambaye ni Songoro Marine anaendelea na ujenzi wa vivuko vipya katika karakana yake mkoani Mwanza kwa ajili yakupelekwa kwenye maeneo mbalimbali kutoa huduma kwa wananchi.

Aidha, Bashungwa amesema kuwa tayari ameikutanisha TEMESA na Kampuni ya AZAM Marine na kujadili namna bora yakushirikiana kwa pamoja kuboresha utoaji huduma ya usafiri wa vivuko katika eneo la Magogoni – Kigamboni.

“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan tumejipanga vizuri kuhakikisha tunaboresha vivuko na tutaweka machaguo kwa abiria ambapo watakuwa na chaguo.

“Ukitaka kutumia kivuko cha TEMESA sawa au ukitaka cha AZAM muda mchache kuvuka kwasababu zile ni ndogo siyo kama kivuko kikubwa ambacho unasubiri kupakia magari na abiria ili muweze kuondoka pamoja,” amesisitiza

Bashungwa amesema Wizara inatambua changamoto ya wananchi ni huduma bora ya vivuko nakusema kuwa kuanzia mwezi Agosti mwaka huu wataanza kutekeleza mpango huo utakaotoa wigo kwa wananchi kuchagua huduma wanayotaka kutumia.

“Wapo wanaotaka kushinikiza ili utaratibu na mwelekeo uende kama wanavyotaka wao, sisi hatuendi hivyo”amesema Bashungwa huku akisema kuwataja watu hao ni kuwapa sifa.