Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Serikali imezitaka Taasisi na Mashirika mbalimbali kujitoa kwa jamii hasa katika vituo vya afya vyenye uhitaji zaidi vilivyo pembezoni mwa mji na vyenye wagonjwa wengi.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Selemani, wakati akipokea vifaa Tiba vilivyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kituo Cha Afya Cha mama na mtoto, Nguvu kazi katika Kata ya Chanika Jijini Dar es Salaam.
“Jambo walilolifanya leo TRA ni matendo ya huruma, wanakusanya kodi kwa jamii na wamerudisha kwa jamii, na leo wamekuja kuleta vifaa tiba na vifaa mbalimbali vitakavyotumika katika kituo hiki Cha afya Chanika “
Amewashukuru TRA kwa kutoa kutoa msaada huo wa vifaa hivyo kwani kwa kufanya hivyo wanaendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
“Tunashukuru sana TRA kwa kuweza kukiona kituo hiki Cha Chanika ambacho kipo pembezoni kabisa ya mji, ni kituo Cha Afya lakini kinabeba wananchi wengi, wakazi wengi wa Wilaya ya Ilala ni wakazi ambao wanakaa katika Kata hii ya Chanika, Zingiziwa, Msongola na Gongolamboto ambao wengi wanakitegemea kituo hiki Cha Chanika”
Pia amewataka TRA kuendelea kukusanya mapato na kufanya maendeleo ili kufikia malengo.
Kwa upande wake Meneja wa Mkoa wa Kodi Ilala, Masau Malima amesema vifaa walivyopeleka katika hospitali hiyo vina thamani ya Shilingi 7, 649, 100 ambapo miongoni mwa fedha hizo zipo ambazo zimetoka mifukoni mwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Ilala na Mfuko wa Mkoa.
“Hata mtumishi mmojammoja ameguswa kwa namna ambavyo anaweza akachangia maisha ya mama na mtoto”
Malima amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa maelekezo thabiti kwa Mamlaka yetu na maelekezo ya baraza la mawaziri ambayo kwa kiasi kikubwa yameendelea kuimarisha hali ya uchumi, ukusanyaji kodi na kuongezeka kwa Kasi kubwa kwa mapato ya serikali kwa ujumla.
Kadhalika Malima amewataka wale wote wanaotakiwa kulipa mapato yao kulipa mapato hayo kabla ya tarehe 31 Desemba mwaka huu.
Naye Mganga mfawidhi wa kituo Cha Afya kinachohudumia mama na mtoto, Chanika Dkt. Hezron Liyange, ameishukuru serikali kwa kuwawezesha TRA kuweza kuwapatia vifaa hivyo ambapo pamoja na vifaa hivyo walivyopata bado Wana uhitaji mkubwa wa vifaa hivyo kwani wanatarajia kuongeza wodi ya watoto wachanga.
Akifafanua kuhusu takwimu za wagonjwa wanaofika kituoni hapo, Malima alisema kwa siku wagonjwa wanaowahudumia ni 200-300 , kwa upande wa akina mama wanaojifungua ni 40-100 kwa siku, kwa mwezi wakina mama pekee wanaoingia wodi ya wazazi ni 700-1000 na wanaojifungua hapohapo ni 800-900 lakini pia wapo watoto robo tatu yao wanahitaji huduma za dharura kutokana na kuwa na changamoto kadhaa hivyo imepeleka uhitaji wa vifaa kuwa mkubwa Hospitalini hapo.
More Stories
DC Mgomi ataka wahitimu Jeshi la Akiba kuwa macho ya Serikali
Viongozi,Makada CCM kufanya ufunguzi kampeni Serikali za Mitaa
Wadau wachangia vifaa Kariakoo