January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Suleiman Massoud Makame, Wazara wa  Uchumi wa Blu,

Serikali yawataka madereva kupakia abiria katika vituo vinavyotambulika

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Zanzibar

WAZIRI wa Wizara ya  Uchumi wa Blu, Suleiman Massoud Makame amewataka  madereva wa gari za abiria pamoja na waendesha bodaboda kupakia abiria katika vituo vilivyowekwa kisheria ili kuepusha ajali za kizembe.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya  lami salama Mkoa wa Kaskazini Unguja iliyofanyika katika Uwanja wa Misuka Mahonda amesema kitendo cha madereva kupakia abiria katika vituo visivyokuwa rasmi ni miongoni mwa sababu zinazosababisha ajali zinazosababisha vifo pamoja na ulemavu.

Aidha ameiomba Wizara ya Mawasiliano kuanzisha vituo vya daladala pamoja na kuweka alama za barabarani ili kupunguza idadi ya ajali katika mkoa huo pamoja na kuwasisitiza wananchi kutumia vituo vilivyoekwa kisheria.

Waziri Suleiman amesema barabara ni kiunganishi kikubwa cha shughuli mbalimbali za kijamii ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa kichocheo kizuri cha kuleta maendeleo hivyo ipo haja kwa kila mtumiaji kuhakikisha anazingatia matumizi sahihi ya barabara ili kila mmoja aweze kutimiza malengo yake.

Vilivile amewataka madereva hao kuacha tabia ya kumwaga mafuta machafu katika barabara kwani kufanya hivyo kunasababisha kuharibika kwa miundombinu hiyo ambayo serikali imetumia gharama kubwa kuzitengeneza.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud amesema uongozi wa mkoa huo utahakikisha unasimamia kwa kuwachukulia hatua za kisheria madereva watakaobainika kupakia abiria kinyume nataratibu ziliwekwa kisheria pamoja na kutokuwa na leseni ya chombo hicho.

Aidha amewataka madereva wa bodaboda pamoja na gari za abiria kukata bima za vyombo vyao ili kuendesha shughuli zao bila ya usumbufu wowoye.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja mkaguzi wa Jeshi la Polisi, Mohammed Maulid Khalifa amewataka madereva hao kuzingatia sheria na alama za barabarani pamoja na kuahidi kushirikiana na uongozi wa mkoa huo katika mikakati ya kudhibiti ajali za barabarani.

Uzinduzi wa Kampeni ya Lami Salama Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na zoezi la ugawaji wa kofia ngumu kwa madereva wa bodaboda umeratibiwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na Shirika la Bima Zanzibar, ambapo jumuiya na taasisi mbali mbali zilishiriki katika kampeni hiyo ikiwemo jumuiya ya gari za mchanga, jumuiya ya gari za abiria na viongozi mbalimbali wa chama na serikali mkoa wa kaskazini unguja wameshiriki katika kampeni hiyo.