October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yawaonya wamiliki wa maduka ya dawa

Na Irene Clemence,TimesMajira Online, Dar

SERIKALI imewataka wamiliki wa maduka ya dawa za binadamu kuacha kutoa dawa kwa mgonjwa ambaye ana cheti cha daktari au tabibu kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria zilizowekwa.

Mfamasia Mkuu wa Serikali Daud Msasi akitoa ufafanuazi wa mambo kadhaa katika uzinduzi huo jijini Dar es Salaam.

Pia imewaomba wananchi kuhakikisha watumia dawa kwa uangalifu na umakini zaidi ili kuweza kuepuka usugu wa vimelea dhidi ya dawa aina ya antibayotiki.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Abel Makubi alipokuwa akizindua maadhimisho ya wiki ya kuhamasisha wananchi kuhusu uelewa wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa aina ya antibayotiki.

Mganga Mkuu wa serikali Profesa Abel Makubi akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya kuamasisha wananchi kuhusu uelewa wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa aina ya Antibayotiki

Amesema, baadhi ya maduka ya dawa yamekuwa yakifanya makosa kwa kumpatia mgonjwa dawa bila ya kuona cheti kilichotolewa na daktari.

“Cheti cha daktari ni muhimu kwa mgonjwa kuwanacho kabla kupewa dawa ya aina yoyote iwe katika kituo cha huduma ya afya au duka la dawa,”amesema Profesa Makubi.

Amesema, kutolewa kwa dawa hizo kiolela bila ya kuona cheti cha daktari kinaweza kumsabisha mgonjwa usugu wa vimelea vya dawa.

Amesisitiza kuwa, uwepo wa usugu wa vimelea vya katika dawa Antibayotiki unaweza kuliweka taifa katika kupoteza nguvu kazi pamoja na kutumia fedha nyingi kutumia kununua dawa.

Profesa Makubi amesema, kutokana na matumizi mabaya ya dawa hizo kwa tiba ya binadamu na wanyama madhara yake yamekuwa makubwa ya kutisha.

Amesema, kwa mujibu wa tafiti zimeonesha kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa za matumizi ya dawa hizo kutumika isivyo sahihi.

“Asilimia 50 ya dawa zimekuwa zikitumika isivyo sahihi huku matumizi makubwa kutibia mifugo na kuchaganywa katika vyakula vya wanyama kinyume na taratibu za kitabibu,”amesema Profesa Makubi.

Ameongeza kuwa, ripoti ya benki ya dunia ya mwaka 2017 inabainisha kuwa zaidi ya watu laki 7 wanafariki Kila mwaka kutokana na usugu wa dawa hizi.

Akizungumza kuhusu utumiaji wa dawa kwa mgonjwa alisema anapaswa kufuata maelekezo ya dawa sahihi ikiwa ni pamoja na kuepuka kukatisha dozi.

“Kila mtu anapaswa kufuata matumizi sahihi ya dawa ikiwa ni pamoja na kutozitumia kiolela ikiwa ni pamoja na kutokukatisha dozi “amesema Profesa Makubi

Kwa upande wake Mfamasia Mkuu wa Serikali Daud Msasi amrsema kwa sasa wanafanya utaratibu wa kupitia maduka yote kama njia ya kujiridhisha katika utoaji wa dawa.

Aidha alitaka jamii kuacha kutumia dawa ambazo mtu tayari amezitumia kwani kufanya hivyo kinaweza kusababisha usugu wa dawa.

Pia amesema kupitia wiki hii wanaendelea kutoa elimu ya uelewa juu ya matumizi sahihi ya dawa aina ya Antibayotiki ili siweze kusababisha vimelea vya usugu dhidi ya dawa hizo.