Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
SERIKALI imewahimiza wazazi na walezi kusimamia malezi na elimu ya watoto ili wawe na maadili mema huku ikieleza kuwa haina dini hivyo itaendelea kushirikiana na madhehebu yote ya dini na kuwahudumia wananchi kwa haki.
Pia itasimamia ukusanyaji wa kodi na itawaunga mkono wafanyabiashara wanaofanya biashara kwa kuzingatia sheria,haitakuwa radhi na wanaokwepa kulipa kodi kwa kuwa kulipa ni wajibu.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda,amesema Aprili 11,2024 wakati akizungumza katika Baraza la Eid El Fitr,lililofanyika katika Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BOT),jijini Mwanza.
Amesema serikali itawahudumia kwa haki wananchi wa madhehebu yote na wasio na dini,katika kujenga maadili mema kwa vijana,wazazi na walezi watimize haki na wajibu wao wa kusimamia malezi bora ya watoto kwani maadili huanzia nyumbani.
“Niwakumbushe wazazi na walezi,mmesahau kutimiza haki na wajibu wa malezi ya watoto,jamii bora itajengwa na vijana bora, hawawezi kupatikana kama hawana malezi bora,hivyo,wazazi na jamii mnawajibika kuwajenga vijana na kuwafanya wawe na adabu,”amesema Mtanda na kuongeza;
“Tusimamie elimu na maadili mema kwa vijana na watoto wetu,mtu yeyote aliyekosa elimu na adabu ni yatima,tusiwafanye vijana yatima kwa kukosa elimu na adabu,tuwape elimu ambayo ni kichocheo cha maisha bora ya binadamu aliyeandaliwa vizuri.”
Mkuu huyo wa Mkoa amesema vijana (Waraibu) wanaotumia dawa za kulevya wengi walikosa malezi ya wazazi wote wawili wakihangaika kutafuta fedha nyingi na kusahahu wajibu wao huku wasichana wa kiislamu wasijiingize na kuona fahari kujiita single mother.
Amesema kufunga katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuna faida moja ni kumcha Mungu na nyingine za kidunia ikiwemo kutunza afya,kuimarisha upendo na uhusiano miongoni mwa waislamu,kuwafanya wakarimu hasa wasio waislamu na mikusanyiko hiyo imeleta neema kwa watu wengine.
Ameipongeza BAKWATA Mwanza na waislamu,kujenga vituo vya afya hivyo atatoa ushirikiano hadi vikamilike.
“Muumini mwenye afya njema mbele ya Mungu ni bora kuliko mdhaifu.Sura al-Baqarah aya ya 10 inasema; kuna watu wana maradhi katika nafsi zao,wana macho lakini hawaoni,wana masikio hawasikii.Tuwe miongoni mwa watu wanaosikia yale yanayosemwa na viongozi wetu,tuyapokee na kuyazingatia,”amesema Mtanda.
Amesema kulipa kodi ni wajibu na hata zamani ilikuwepo hivyo si suala la Rais kwani nchi isiyokusanya kodi kiuchumi italega lega hivyo atasimamia hilo mkoani Mwanza.
“Katika utendaji wangu sina mpambe,mpambe ni utendaji wangu,nitasimamia ukusanyaji wa kodi kwa haki,wakwepa kodi hao si rafiki zangu,lakini wanaodhulumiwa na kutaka kufunga biashara na wako tayari kulipa kodi nitawaunga mkono,”amesema Mtanda.
Awali Sheikh wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hasani Kabeke,amesema BAKWATA ni daraja kati ya waislamu na serikali ,hivyo siku ya Baraza la Eid ni siku ya serikali kuelekeza masuala mbalimbali yanayohusu wananchi.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua