June 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yawahakikishia upatikanaji Umeme Wakazi wa Kitongoji cha Orera – Moshi Vijijini

‎Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

‎SERIKALI imetoa hakikisho la kuwasha matumaini kwa wakazi wa Kitongoji cha Orera, kilichopo katika Kijiji cha Mweka, Kata ya Kibosho Mashariki, Jimbo la Moshi Vijijini, kuwa huduma ya umeme itawafikia hivi karibuni kupitia mkakati wa kitaifa wa usambazaji wa umeme vijijini.

‎Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi, bungeni jijini Dodoma.

Mbunge huyo alitaka kujua ni lini Serikali itaunganisha huduma ya umeme kwa wakazi wa Kitongoji cha Orera ambao bado hawajanufaika na huduma hiyo.

‎””Lini Serikali itawaunganishia umeme wananchi wa Kitongoji cha Orera, Kijiji cha Mweka, Kata ya Kibosho Mashariki?” aliuliza Prof. Ndakidemi.

‎Akijibu swali hilo, Kapinga amesema kuwa katika Jimbo hilo kuna mkandarasi ambaye tayari yupo eneo la kazi akiendelea na utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji 15 vilivyopangwa katika kila jimbo, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuongeza upatikanaji wa nishati vijijini.

‎“Na kiitongoji hicho pia kipo katika mradi huo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa mkandarasi yupo site, anaendelea na kazi ya upimaji, na wananchi wa Kitongoji cha Orera wataanza kupata huduma ya umeme hivi karibuni,” alisema Kapinga.

‎Kwa mujibu wa Serikali, miradi hii inalenga kuhakikisha kuwa kila mwananchi anafikiwa na huduma ya nishati bora na salama, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kitaifa ya kufikisha umeme kwa asilimia 100 ya Watanzania ifikapo mwaka 2030.

‎Prof. Ndakidemi, kwa upande wake, aliipongeza Serikali kwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa lakini alisisitiza umuhimu wa kasi ya utekelezaji kuongezwa, hasa katika maeneo ya vijijini ambako bado kuna mahitaji makubwa ya nishati kwa matumizi ya nyumbani, kilimo, biashara ndogondogo, na taasisi za kijamii.

‎“Nia ya wananchi wa Moshi Vijijini ni kuona huduma hii inawafikia kwa haraka. Wana matumaini makubwa na mradi huu wa kitaifa, na tunaiomba Serikali ihakikishe hakuna kitongoji kinachobaki nyuma,” amesema Prof. Ndakidemi.

‎Kwa sasa, Serikali inaendelea kusambaza umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano na TANESCO katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni juhudi za kuhakikisha nishati inakuwa kichocheo cha maendeleo ya watu.