December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatumia bil. 6/- miradi ya maji Mkalama

Na Mwandishi Wetu, timesmajira,online

SERIKALI imetumia zaidi ya sh. bilioni 6.318 kwa ajili ya ujenzi wa miradi kwenye vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Mkalama, mkoani Singida ili kuwaondolea adha ya maji safi wananchi wake.

Hayo yamesemwa jana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wananchi waliohudhuria mkutano wa kuwanadi wagombea ubunge na udiwani wa CCM uliofanyika kwenye viwanja vya stendi ya mabasi Gumanga, wilayani Mkalama.

Majaliwa ambaye alikuwa mkoani Singida kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Magufuli, alisema Serikali ya awamu ya tano imejenga miradi ya kimkakati zaidi ya 1,490 kwenye sekta ya maji nchi nzima.

Akifafanua baadhi ya miradi iliyofanyika katika kipindi cha mwaka 2015/2016 na 2019/2020, Majaliwa amesema kati ya fedha hizo, sh. bilioni 1.37 zimetumika kwa ajii ya mradi wa maji vijiji vya Mughano, Ngimu, Mgori, Malolo, Kijota, Ghaluyangu na Mangida.

“Miradi mingine ni mradi wa maji kijiji cha Mwankoko ‘B’ ambao umetumia sh. milioni 656, na mradi wa maji kijiji cha Kisaki ambao umetumia sh. milioni 551. Pia, sh. milioni 428 zimetumika kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa maji kijiji cha Gumanga na sh. milioni 910 zimetumika kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa maji kijiji cha Nyahaa,” alisema.

Akifafanua zaidi, Majaliwa amesema sh. milioni 341 zimetumika kwa ajili ya mradi wa uchimbaji wa visima virefu saba katika maeneo ya Nduguti, Kisuluiga, Matongo, Ipuli, Mkiko, Mwanga, Wangeza, Kinampundu, Kinyangiri, Msingi, Senene, Milade, Mbigigi, Nduguti (visima viwili), Tumuli (kisima kimoja) na Ibaga (kisima kimoja).

Amesema sh. milioni 158 zimetumika kwa ajili ya mradi wa uboreshaji maji katika kijiji cha Nduguti na sh. milioni 70 zimetumika kwa ajili ya uboreshaji maji katika kijiji cha Kinyangiri.

Mbali ya juhudi zote hizo, Majaliwa amesema sh. bilioni 1.37 zimetumika kwenye mradi wa maji kwa vijiji 10 vya Ibaga, Lyelembo, Mpambala, Ikolo, Kinyambuli, Ipuli, Makuro, Donimic, Ishinsi Nkalalala na Lukomo.

Wakati huo huo, Majaliwa alisema sh. milioni 235.98 zimetumika kwa ajili ya uchimbaji wa visima visima virefu na vifupi 20 ikiwa ni pamoja na ufungaji wa pampu za mkono.

Amesema kiasi kingine cha sh. milioni 144 kimetumika kwa ajili ya upanuzi wa mradi wa maji kijiji cha Mntamba na sh. milioni 85 nyingine zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa mradi wa maji kijiji cha Ipuri.