November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatoa viwanda vyake 10 viendelezwe

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

SERIKALI kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imekabidhi kwa taasisi nne viwanda 10 ambavyo wawekezaji wake walishindwa kuviendeleza kulingana na mikataba ya mauzo na hivyo malengo ya serikali ya kubinafsisha viwanda hivyo kutotimia.

Taasisi zilizokabidhiwa viwanda hivyo ni Mamlaka ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo (SIDO) na Bodi ya Mazao Mchanganyiko (CPB). 

Agosti, mwaka jana Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, wakati huo, alitangaza na kutoa maelekezo kuhusiana na Viwanda 20 vilivyorejeshwa serikalini na kusema viwanda 10 vihamishiwe katika Taasisi za umma na Viwanda 10 vitafutiwe wawekezaji wengine kwa njia ya zabuni.

Akikabidhi viwanda hivyo jana jijini Dar es Salaam, Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto aliwapa wakuu wa taasisi hizo wiki tatu kuhakikisha kwamba wanawasilisha mpango kazi ambao utafuatiliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

“ Ingawa leo (jana) nawakabidhi viwanda hivyo, mnatakiwa kuwasilisha mipango mikakati yenu ya kuendeleza viwanda hivi ifikapo Juni 20 mwaka huu,“ alisema Benedicto na kuongeza kuwa,  mipango hiyo ya uwekezaji watakayowasilisha ndiyo itatumika na Ofisi ya Msajili wa Hazina kufanya zoezi la ufuatiliaji na tathmini juu ya utekelezaji wake.

Viwanda 10 ambavyo vimeelekezwa kuhamishiwa katika taasisi hizo ni TPL Shinyanga Meat Plant ambacho ni cha nyama, Mafuta Ilulu (Lindi), kiwanda cha kubangua korosho cha Nachingwea Cashewnut (Lindi), Mkata Sawmill Limited na Sikh Sawmill Limited (Tanga), National Steel Corporation cha Dar es Salaam na  Mbeya Ceramic Ltd. Vingine ni Mang’ula Mechanical & Machine Tools (Morogoro), Mwanza Tanneries (Mwanza) na TPL Mbeya.

“Kati ya Viwanda hivyo, Kiwanda cha Mang’ula Mechanical & Machine Tools kitahamishiwa NDC, Kiwanda cha Mbeya Ceramic kinakwenda SIDO na Viwanda vinane vilivyobaki vinahamishiwa EPZA,” alisema Msajili wa Hazina, Benedicto.

Aliwataka viongozi wa taasisi hizo kuhakikisha kwamba wanatimiza malengo ya uwekezaji yakiwemo ya kuongeza uzalishaji, mapato kwa serikali, ajira, kuingiza teknolojia mpya katika sekta ya viwanda na uzalishaji na hatimaye kupunguza umasikini nchini.

Akifafanua zaidi alisema Kiwanda cha Mang’ula Mechanical & Machine Tools kinakabidhiwa NDC, na  SIDO wamekabidhiwa Mbeya Ceramic huku viwanda saba vimekabidhiwa EPZA.

Viwanda vilivyokabidhiwa EPZA ni TPL Shinyanga Meat Plant, Mafuta Ilulu, Nachingwea Cashewnut, Mkata Sawmill Limited, Sikh Sawmill Limited, National Steel Corporation na TPL Mbeya.

Aidha Msajili Benedicto alisema Kiwanda cha Mwanza Tanneries, Msajili atakabidhi viwanja vitatu (Na. 2,4, na 5) kati ya vitano  vilivyopo kwenye eneo hilo.

“Eneo lililobaki linasubiri maelekezo kutoka kwa Mamlaka kabla ya kukabidhiwa rasmi kwa kuwa kulikuwa na maelekezo mengine ambayo yalitakiwa kukamilishwa kabla ya kufanya makabidhiano rasmi na EPZA” alisema.