January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatoa muongozo kuhusu Corona shuleni

Na Joyce Kasiki,TimesMajira Online

WIZARA ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto imefanyia maboresho ya muongozo mashuleni na vyuoni ili kukidhi mahitaji ya sasa ya kuwakinga wanafunzi na maambukizi ya virusi vya corona huku ikihimiza wakuu wa taasisi hizo kuhakikisha inauzingatia.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa,Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Profesa Abel Makubi amesema kuwa, wasimamizi wote wanapaswa kuuzingatia muongozo huo na kuutekeleza ipasavyo ikiwemo kuweka vyombo maeneo mbalimbali ili wanafunzi waweze kunawa kwa maji tiririka na sabuni lakini kuhimiza matumizi ya barakoa kwa wanafunzi.

“Mwaka jana tulitoa muongozo huu ,inawezekana ,matumizi ya vifaa hivi yalipungua au yalisitishwa kabisa,sasa tunaagiza miundombinu ya maji ya kunawa irudishwe na itumike kama kawaida,wanafunzi wawe na barakoa angalau mbili au tatu ambazo zitamwezesha kufua na kubadilisha,”amesema Profesa Makubi na kuongeza kuwa,

“Vile vile tunaagiza wasimamizi hao wa taasisi za elimu zikiwemo shule na vyuo waimarishe mifumo ya maisha kwa kufanya ukaguzi na usafi wa mara kwa mara katika madarasa na mabweni, lakini pia wafanye ukaguzi wa afya za wanafunzi na kutoa taarifa haraka kwa vyombo vinavyohusika na kwa utaratibu usitia hofu mara wanapoona mwanafunzi ana kiashiria cha kuugua corona,”amesema.

Aidha, Profesa Makubi amewataka viongozi wote wa mikoa na wilaya kuongeza kasi ya udhibiti na kuhakikisha barakoa zinavaliwa wakati wote watu wanapoingia kwenye taasisi za Serikali.

Vile vile amewataka viongozi wa dini kuendelea kuelimisha waumini wao katika nyumba za ibada kuhusu kujikinga na ugonjwa huo na kufuata taratibu zote za kujikinga kwa mujibu wa miongozo ambayo imeshatolewa na serikali .

“Tangu ugonjwa huu umeingia tumeshatoa miongozo 16 ambayo inatakiwa kufuatwa kwa ajili ya kujikinga na corona tunaomba kasi hii ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huuu iongezeke kwa vongozi wetu wa dini Tunaomba viongozi wa dini watekeleze,”amesema Katibu Mkuu huyo.

Ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kufuata miongozo na taratibu za kujikinga na ugonjwa huo kwa kuepeuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima, lakini pia kujiongoza wenyewe hasa kwa wale wanaotumia usafiri wa daladala.

“Elimu hii imeshatolewa sana,wananchi wajiongoze wenyewe usikubali kukaa kwenye mikusanyiko ,lakini pia hata kwenye daladala usisubiri mpaka uambiwe usipande daladala iliyojaa watu,wewe mwenyewe ukishaona daladala imejaa usipande ,subiri nyingine,”amesisitiza.

Pia amewaasa wananchi kujenga tabia ya kufanya mazoezi lakini pia kula chakula bora ili kuongeza kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo corona.

Aidha, amewataka viongozi wote wa wilaya na mikoa kuwa mfano wa kuigwa kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na Wizara yake kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo ili wananchi nao waweze kuiga kutoka kwao.

“Siku zote tunasema kiongozi ni mfano,sasa kiongozi wakati unatoa maelekezo lazima na wewe uwe mfano wa kutekeleza maelekezo hayo,”amesisitiza.