June 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali Yatoa Majibu Kuhusu Upatikanaji wa Umeme Vitongoji vya Jimbo la Mwibara

‎Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

‎ SERIKALI  imewahakikishia  wakazi wa Jimbo la Mwibara kuwa mpango wa kupeleka umeme katika vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na huduma hiyo unaendelea kutekelezwa, huku ikieleza kuwa utekelezaji wake unategemea upatikanaji wa fedha.

‎Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nishati Judithy Kapinga  kufuatia swali la Mbunge wa Mwibara,  Charles Kajege, aliyehoji ni lini serikali itapeleka umeme katika vitongoji ambavyo bado havijanufaika na huduma hiyo muhimu ya kijamii.

‎”Jimbo la Mwibara bado lina vitongoji vingine ambavyo havina umeme. Je, lini Serikali itapeleka umeme katika vitongoji hivyo?” alihoji  Kajege.

‎Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nishati,  Kapinga, amesema kuwa pamoja na miradi inayoendelea kutekelezwa katika baadhi ya vitongoji vya Jimbo la Mwibara, eneo hilo pia limepangwa kunufaika na awamu ya pili ya mradi mkubwa wa kupeleka umeme kwenye vitongoji, unaojulikana kama Awamu ya Pili B.

‎“Jimbo la Mwibara nalo limetengewa vitongoji katika mpango huo. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itaendelea kupeleka umeme kwenye vitongoji vya Mwibara kadri ya upatikanaji wa fedha,” alisema Kapinga.

‎Aliongeza kuwa lengo kuu la Serikali kupitia Wizara ya Nishati ni kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anafikiwa na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030, na kuwa jitihada zinaendelea kuhakikisha kuwa maeneo ya vijijini, yakiwemo yale ya Mwibara, hayabaki nyuma katika maendeleo ya nishati.

‎Jimbo la Mwibara, lililopo katika Mkoa wa Mara, limekuwa likikua kwa kasi katika sekta mbalimbali za maendeleo, lakini bado linakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya umeme hasa katika baadhi ya vitongoji vya pembezoni.

‎ Wakazi wa maeneo hayo wamekuwa wakilalamikia hali hiyo kwa muda mrefu, wakitaka hatua za haraka zichukuliwe ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

‎Kwa upande wake, Mbunge Kajege ameipongeza Serikali kwa hatua zinazochukuliwa, lakini amesisitiza kuwa kasi ya usambazaji wa umeme inapaswa kuongezwa ili kuendana na matarajio ya wananchi.