December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatoa maelekezo aliyefunga taa manispaa ya Bukoba

Na  Ashura Jumapili,Bukoba,

Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Albert Chalamila,ametoa maelekezo kwa mkandarasi aliyefunga taa katika mradi wa maegesho ya maroli uliopo Kata Ijuganyondo iliyopo Manispaa ya Bukoba kubadilisha  mara moja taa hizo kwa sababu ikifika usiku taa hizo zinakuwa zinafifia.

Chalamila,alitoa maelekezo hayo alipofika katika eneo hilo kwaajili ya kukagua mradi na kuweka jiwe la msingi katika mradi huo  mkubwa wenye uwezo wa kuegesha Maroli 30 kwa wakati mmoja.

Amesema  nyakati za usiku taa hizo hazina mwanga,hivyo zinapaswa kubadilishwa kama mkandarasi aliyeziweka akiona ugumu kuzibadilisha maelekezo ya pili ni kwa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU )ifanye kazi ya kukagua mradi huo kwa ujumla ili kuweza kubaini mkataba ulitaka taa za aina gani zifungwe eneo hilo

Amesema Manispaa ya Bukoba imetumia gharama kubwa kununua eneo hili na kulipa fidia kwa wananchi kwa sababu hawana maeneo makubwa ya wazi  yanayoweza kuhimili uwekezaji mkubwa kama huu wa maegesho ya Maroli uliowekezwa na Rais wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan.

“Nitoe  ushauri mstahiki Meya baraza la madiwani na madiwani wao waanze mkakati wa haraka kuweza kupanua mipaka ya Manispaa ya Bukoba ,tungekuwa na maeneo makubwa tusingehangaika kununua maeneo ya wananchi na kulipa fidia hizo milioni 200 ni pesa nyingi”amesema Chalamila.

Amesema Rais Samia amejipanga kuleta miradi mingi ya maendeleo katika manispaa ya Bukoba “ninaiona hatari ya moja kwa moja miradi hiyo kushindwa kutekelezeka kwa haraka  kama upatikanaji wa maeneo utakuwa kikwazo”anasema Chalamila.

Mkuu wa Idara ya viwanda,uwekezaji na biashara Manispaa ya Bukoba Philibert Gozbert akisoma taarifa ya mradi wa uwekezaji ya kituo Cha maegesho ya maroli kwa mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila

Amesema Rais Samia amejipanga kuifumua upya Manispaa ya Bukoba ili iwe na hadhi kubwa kama manispaa nyingine zenye hadhi kubwa za ndani na njen ya nchi.

Awali akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa Mkuu wa Idara ya Viwanda,Biashara na Uwekezaji Manispaa ya Bukoba, Philbert  Gozbert ,amesema  ujenzi  wa mradi huo awamu ya kwanza ulianza kutekelezwa Agost 5,2022 na kukamilika Desemba Mosi, 2022 kwa gharama ya zaidi ya  shilingi milioni (  475.5  ).

Gozbert,amesema malipo ambayo yameshafanyika ni zaidi  ya shilingi milioni (  448.5 )bado shilingi milioni (23.6 )ambazo ni fedha za matazamio ( Retention Money ).

Amesema miundombinu iliyojengwa kwenye mradi huo ni choo chenye matundu manne ,bafu mbili,uzio wenye milango miwili mmoja wa kuingia na kutoka ,jengo la mlinzi na mtoza ushuru.

Amesema  eneo la kuegesha maroli linauwezo wa kuegesha maroli 30 kwa wakati mmoja ,taa 20 za Wats 150,ujenzi wa miundombinu ya Maji ya Buwasa umekamilika pia lipo tanki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 2,000 litakalotumika endapo maji yatakatika.

Amesema malengo ya ujenzi wa mradi huo ni kuboresha huduma za kuegesha maroli,kuzuia uharibifu wa barabara  unaosababishwa na magari makubwa ya mizigo,kuondoa usumbufu wa magari makubwa yaliyokuwa yanaleta mizigo mjini na kuegeshwa popote kwaajili ya kushusha bila mpangilio,kuongeza mapato ya ndani kutokana na fedha zitakazokusanywa katika mradi huo.

Amesema malengo mengine kupanua Manispaa ya Bukoba ,kuongeza fursa za uwekezaji  na kuongeza ajira.