Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele, amesema serikali imeipatia mamlaka hiyo kiasi cha shilingi Bilioni 1, ili kuboresha hali ya huduma ya maji kwenye maeneo ya pembezoni mwa Jiji hilo.
Hivyo ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji Jiji la Mwanza.
Akizungumza jijini hapa Mhandisi Msenyele amesema serikali kwa kutambua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama inayowakabili wananchi waishio maeneo ya pembezoni mwa Jiji la Mwanza hususan maeneo ya milimani imeamua kutoa fedha hizo ili kuboresha huduma.
Amesema, kwa juhudi na ubunifu wa Rais Samia wamepata fedha za kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo yenye changamoto.
Ambapo fedha hizo zimepatikana kupitia programu maalum ya utekelezaji wa miradi kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.
“Tunamshukuru Rais wetu,kwa ubunifu wake wa kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha kuhakikisha miradi inatekelezeka,kupitia fedha hizi tumeweza kuyafikia maeneo matano yaliyokuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji,”amesema Mhandisi Msenyele.
Hata hivyo Mhandisi Msenyele anaeleza kuwa taratibu za kuainisha maeneo yenye changamoto ya maji zilifanyika kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za Mitaa, Madiwani, Wabunge wa Jimbo la Nyamagana na Ilemela.
Ameyataja maeneo hayo kuwa ni Mlima wa Rada na Nyamhongolo kwa upande wa Wilaya ya Ilemela huku Wilaya ya Nyamagana ikiwa ni Ihila- Buhongwa, Luchelele-Mnangani na Kambarage.
Ameeleza kuwa uteuzi wa maeneo hayo umezingatia hali halisi ya kijiografia kwani maeneo hayo ni ya milima ambapo miundombinu ya MWAUWASA iliokuwepo haikuweza kufikisha huduma.
“Mwanza maeneo mengi yapo mlimani mifumo yetu haikuwa na uwezo wa kufika kwenye maeneo haya lakini kupitia hizi fedha tunajenga miradi ambayo inakwenda kuondoa changamoto hiyo,”amesema Mhandisi Msenyele.
Aidha ameeleza kuwa utelekezwaji wa mradi kwa sasa upo asilimia 40 na utakamilika Aprili, 2022.
More Stories
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi
SACP Katabazi: Elimu ya usafirishaji wa kemikali bado ni muhimu kwa watanzania