Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online
Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo J. Dugange(Mb) amesema Katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali imetenga shilingi bilioni 17.1 kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali 19, hadi kufikia mwezi Februari, 2023 kiasi cha shilingi bilioni 12.95 zimekwishatolewa kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya hospitali Kongwe kumi na nne.
Amesema hayo leo tarehe 11 Aprili 2023 Bugeni Dodoma wakati akijibu Swali la Mbunge Viti Maalum, Mhe. Lucy John Sabu aliyetaka kujua Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya ukarabati wa miundombinu ya Hospitali ya Mji wa Bariadi.
Dkt. Dugange amesema Serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali Kongwe nchini ikwemo Hospitali ya Mji wa Bariadi ambapo hospitali ya Mji wa Bariadi imepelekewa shilingi milioni 900 na kazi za ujenzi zinaendelea
Aidha, Wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, Mhe. Athuman Almas Maige aliyetaka kujua Je, lini barabara ya Manoleo hadi kituo cha Afya Upuge itajengwa kwa kiwango cha lami.
Dkt. Dugange amesema Barabara ya Manoleo – Kituo cha Afya Upuge yenye urefu wa kilomita 22.10 imesajiliwa kwa jina la Nyambele – Upuge – Muhogwe – Magiri ambapo kutokana na umuhimu wake imeendelea kutunzwa kwa kuwekwa kwenye vipaumbele vya kibajeti.
Amesema Kutokana na umuhimu wa barabara hiyo, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe kilomita 13 na kujenga makalavati saba, ambapo ipo hatua ya uandaaji wa nyaraka za zabuni kwa ajili ya kumpata Mkandarasi. Ujenzi unatarajiwa kuanza mwezi Mei, 2023.
Kadhalika, Dkt. Dugange amesema Serikali inaendelea kutafuta fedha ili barabara ya Nyambele – Upuge – Muhogwe – Magiri yenye urefu wa kilomita 22.10 iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.
More Stories
CP.Wakulyamba ashuka Katavi na Nguzo nne za Uongozi
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Maandalizi ya mkutano mkuu CCM yapamba moto