November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatekeleza miradi ya maji ya Bilioni 2.9 Ngara

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Ngara

SERIKALI ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya sh bil 2.9 kwa ajili ya kutekeleza miradi 5 ya maji katika halmashauri ya Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili juzi Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani humo Mhandisi Simeon Ndyamukama alisema miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Alisema fedha za utekelezaji miradi hiyo zimetolewa na serikali kwa asilimia 100 katika mwaka wa fedha 2021/2022 na miradi yote inatarajiwa kukamilika katika mwaka huu wa fedha 2022/2023.

Alitaja miradi hiyo kuwa ni ule unaaotekelezwa katika kata ya Kabanga kwa fedha za Mfuko wa Barabara kiasi cha sh mil 941 ambao una vyanzo 2, chemchem na kisima kirefu.

Mhandisi Ndyamukama alifafanua kuwa mradi huo unatarajiwa kunufaisha wakazi zaidi ya 10,000 wanaoshi katika vijiji 3 vya Murukukumbo, Kumuzuza na Kabanga katika kata ya Kabanga na utekelezaji wake umefikia asilimia 30.

Alisema katika mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya BF Ghat Ltd ya Jijini DSM watajenga nyumba 2 za mitambo (pumb house), vibanda 3 vya kuchotea maji na ofisi ya watoa wa huduma ya maji (CBWSO’s).

Alitaja miradi mingine kuwa ni Mukariza-Murugina unaotekelezwa katika kata ya Mabawe kwa gharama ya sh mil 371.4 ambapo utekelezaji wake upo katika hatua za umaliziaji, fedha za mradi huo ni za P4R.

Mradi mwingine ni wa Kijiji cha Kasange katika kata ya Kirusha unaotekelezwa kwa fedha za P4R hadi kukamilika unatarajia kugharimu kiasi cha sh mil 283.5 ambazo zitahusisha ujenzi wa vibanda vya kuchotea na nyumba ya mtambo.

Meneja alitaja miradi mingine kuwa ni wa Kijiji cha Kanyinya katika kata ya Mbuba unaotarajiwa kugharimu kiasi cha sh mil 448.1 za mpango wa lipa kwa matokeo (PbR).

Alibainisha mradi mwingine kuwa unatekelezwa katika Vijiji 2 vya Mbuhenge na Kirusha katika kata za Mugoma na Kirusha kwa gharama ya sh mil 941.3 za mpango wa lipa kwa matokeo na mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19.

Wakizungumzia miradi hiyo mkazi wa Kijiji cha Murugina Sebastian Mrukundo na Amina Nzoya wa Kabanga walisema kukamilika kwake kutasaidia kumaliza kilio chao cha miaka kwani tangu nchi ipate uhuru hawajawahi kunywa maji safi na salama ya bomba.

Utekelezaji mradi wa maji katika vijiji vya Muhariza na Murugina utakaogharimu kiasi cha sh mil 371.4 ukiendelea ka kasi kubwa, tenki hilo ni moja ya matenki ya maji ambayo yameanza kujengwa katika kata hiyo ya Mabawe. picha na Allan Vicent.