November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatakiwa kuwapa kipaumbele walimu wanaojitolea.

Na Stephen Noel,Timesmajira
SERIKALI imeshauriwa kuwapa kipaumbele cha ajira walimu waliohitimu mafunzo ya Ualimu ambao wameamua kufundisha kwa kujitolea katika shule za Serikali za Msingi na Sekondari.

Ushauri huo umetolewa na Mdau na Mbobezi wa Masuala ya Elimu
Mwl. Dkt William Hugo Ndimbo alipokuwa akiongea na chombo hiki nyumbani kwake Mjini Mpwapwa.
Dkt Ndimbo alisema kwa sasa shule nyingi za Serikali hapa Nchini zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu hasa zilizoko vijijini, ingawa Vyuo vya Ualimu vya kati na Vyuo Vikuu vikiendelea kutoa Wahitimu (walimu) kila mwaka .

Alisema: “……kiukwel kila mwaka vyuo hivi vimeendelea kutoa Wahitimu (walimu), lakini upungufu wa walimu bado upo, na hivyo kusabanisha utoaji wa Elimu kutokuwa sawa kati ya maeneo ya vijijini na mijini ambako inasadikika angalau kuwepo walimu wengi.”

Swali je, hawa walimu wanaenda wapi baada ya kuhitimu mafunzo yao? Mdau huyo wa Elimu alifafanua kwamba wapo Wahitimu (walimu) ambao wanajiajiri wenyewe katika shughuli mbalimbali zikiwemo ujasiria mali, wapo wanaoajiriwa katika shule binafsi, na wapo wanaofundisha kwa kujitolea katika shule mbalimbali za Msingi na Sekondari husani zilizoko vijijini ambako upungufu wa walimu umekithiri.

Aidha, pamoja na baadhi ya walimu kufundisha kwa kujitolea katika shule hizo, inasikitisha pindi Ajira zinapotoka, walimu hao wanaojitolea pamoja na kuwa na vigezo stahiki hukosa nafasi za Ajira. Inasikitisha zaidi kuona wale wengine waliokuwa labda kwenye Ajira binafsi au shule binafsi ndio hupata nafasi za kuajiriwa. Jambo hili si tu linakatisha tamaa bali kutodumisha dhana halisi ya Uzalendo kwa wale wanaojitolea.
Mdau huyo wa Elimu (Dr. Ndimbo) amesema kwamba ili kudumisha dhana ya Uzalendo kwa vitendo ni vizuri Walimu wote wanaofundisha kwa kujitolea wapewe nafasi kwanza ya ajira, tena kwenye maeneo yale yale wanayojitolea.


Hii itasaidia si tu kupunguza upungufu wa walimu kwenye maeneo/shule hizo bali hata gharama kwa serikali za kuwasafirisha kutoka eneo moja hadi lingine.

Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa upande mwingine imekiri kuwepo kwa upungufu mkubwa wa walimu.
TAMISEM imeeleza kuwa hadi Februari, 2023 ilikuwa na uhitajii wa walimu 362,189 katika Shule za Msingi kwa kutumia uwiano wa 1:45 (Mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45).
Taarifa kutoka TAMISEMI ilifafanua kuwa walimu waliopo ni 175,864 ambao wanafundisha wanafunzi milioni 12.36 waliopo nchi nzima katika ngazi hiyo ya Elimu. Hiyo ni sawa na kusema kwa wastani, mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 70.
Uwiano huo uko juu kuliko mapendekezo ya Serikali ya mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi wasiozidi 45 katika darasa moja.

TAMISEMI iliongeza kuwa ili kuziba pengo hilo wanahitajika walimu 186,325 sawa na asimilia 51.44 au zaidi.
Taarifa ilionesha pia mahitaji ya walimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa shule za msingi ni 4,462 ambapo waliopo ni 1,517 na upungufu ni walimu 2,945 sawa na asilimia 66.

Hata hivyo, taarifa kutoka TAMISEMI ilieleza kwamba tatizo la uhaba wa walimu katika shule za msingi linaweza lisiishe kabisa kwa sababu kila mwaka idadi ya wanafunzi wa darasa la kwanza huongezeka.

Tatizo la upungufu wa walimu sio tu kwa shule za msingi bali linazikumba pia shule za sekondari hasa zinazomilikiwa na Serikali.

Mahitaji ya walimu kwa shule za sekondari hadi kufikia Februari mwaka huu (2024) yalikuwa 174,632.
Waliopo ni 84,700, na upungufu walimu 89,932 sawa na asilimia 51.5.
Mahitaji ya walimu kwa shule za Sekondari yanatokana na ongezeko la TAASUSI (Combinations) za masomo mbalimbali yanayofundishwa, taarifa ya TAMISEMI ilibainisha

Wachambuzi wa Masuala ya Elimu akiwemo Richard Mabala wanasema upungufu wa walimu unawakosesha fursa wanafunzi kupata maarifa na stadi kwa ukamilifu. Hii inawezakuwa kikwazo kwa wanafunzi kufaulu mitihani yao na kumudu maisha yao kwa ujumla.