January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatakiwa kuwajengea uwezo walimu

Na Penina Malundo,timesmajira,online

SERIKALI imetakiwa kuwajengea uwezo na mbinu za ziada  walimu nchini  katika kuwatambua na kuwafundisha watoto wenye Usonji.

Aidha Walimu wakijengewa uwezo  na kupatiwa mbinu hizo za ziada kwa kiasi kikubwa wataweza kuwasaidia Watoto wenye usonji kukaa darasani kwa utulivu,kuelewa  na kutoona kero.

Akizungumza hayo leo jijini Dar es salaam,Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),Dkt. Saidi Kuganda amesema walimu wakiwezeshwa na kujua namna ya kufundisha Watoto wa namna hiyo inasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la Watoto hao.

Amesema ufundishaji wa walimu ni moja ya mbinu ya tiba nzuri ambayo itasaidia kupunguza tatizo la Watoto hao nchini.

“Hatuna data kamili ila tatizo lipo na tunaliona ukiliwahi  mapema  unapunguza kwa kiasi kikubwa madhara yake,ila ukiyaacha na kuchelewa yatakuwa makubwa pindi mtoto anapokuwa,”Amesema

Aidha amesema walimu hao wakiwekewa utaratibu mzuri katika kuwafundisha Watoto hao ni rahisi kuwasaidia katika ukuaji wao.

“Nchi nyingi zinafanya hivyo katika kuhakikisha walimu wanajengewa uwezo na mbinu za ziada za kuwafundisha watoto ikiwemo nchi ya Japan wao wanashughulikia walimu na sio madaktari kwani walimu wanambinu nyingi  za ziada,”alisema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya  Lukiza  Autism,Hilda  Nkabe amesema usonji hauna dawa ila kuna mazoezi tiba ambayo yanasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza makali ya ugonjwa.

Amesema mzazi,mlezi na Familia ya  mwenye mtoto mwenye usonji wanapaswa kuwa na  upendo unaweza kusaidia kupunguza ukali  wa ugonjwa huo kwa mtoto.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Dr.Reginald Mengi ,Shimimana Ntuyabaliwe amesema ni vema jamii kumtambuliza jamii kwa utu wake na sio kwa ulemavu aliokuwa nao.

Amesema utumiaji wa lugha sahihi kwa watu hao itaondioa Imani potofu na kuheshimu utu wa watu wenye ulemavu .