November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatakiwa kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa kazi za staha kwa wafanyakazi wa nyumbani

Na .Judith Ferdinand,Timesmajira online

Imeelezwa kuwa wafanyakazi wa nyumbani ni kundi muhimu sana kwa jamii zetu kwani hufanya kazi ambazo huwezesha ajira nyingine zote kufanyika.

Lakini licha ya umuhimu huo bado ndilo kundi ambalo linanyanyasika zaidi katika jamii hali hii uchangiwa na ukweli kwamba hufanyika katika sekta isiyo rasmi na kuajiriwa kwao mara nyingi hutokea kupitia njia isiyo rasmi ya undugu au mitandao ya madalali.

Hivyo katika kukabiliana na changamoto hiyo watetezi wa haki za wafanyakazi wa nyumbani wanaihimiza serikali kuridhia mkataba wa kimataifa wa kazi za staha kwa wafanyakazi wa nyumbani Namba 189/2011 na kuwepo kwa sheria mahususi kwa ajili ya wafanyakazi wa nyumbani nchini.

Ambapoo hali hiyo imeelezwa kuwa itasaidia kuimarisha mazingira yenye staha kwa wafanyakazi hao na kuwezeshwa usimamizi mzuri wa kisheria kwa masuala yanayohusu wafanyakazi wa nyumbani. Ikumbukwe kuwa ajira ya kazi ya nyumbani ina mazingira fulani maalum na ya kipekee ikilinganishwa na ajira nyingine hivyo yanahitaji sheria mahususi kuwezesha udhibiti na ulinzi sahihi kwa wafanyakazi wa nyumbani.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa nchini mwaka 2016 na Shirika la Kazi Duniani (ILO)ilikadiriwa kuwa kuna wafanyakazi wa nyumbani 883,779 Tanzania Bara na 203,622 Zanzibar,hii inawakilisha asilimia 5 jumla ya watu wenye umri wa kufanya kazi miaka 15-64 nchini Tanzania.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wafanyakazi wa nyumbani ambayo ufanyika Juni 16 ya kila mwaka Meneja wa Nyumba Salama wa shirika la kutetea haki za wafanyakazi wa nyumbani WoteSawa, Jaqueline Ngalo,anaeleza kuwa kundi hilo ni muhimu kwani kitendo cha kufanya uangalizi wa watoto,nyumba na vitu vingine huwafanya waajiri wao kwenda kazini kwao wakiwa na amani kuwa nyumbani pako salama.

Ngalo anaeleza kuwa pamoja na umuhimu huo wa wafanyakazi wa nyumbani bado ndilo kundi la wafanyakazi ambalo linanyanyasika zaidi na kuwa katika mazingira hatarishi.

Anaeleza kuwa wafanyakazi wa nyumbani nchini hapa wanaokabiliwa na mazingira mabaya ya kazi ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa saa nyingi kupita kiasi,kulipwa ujira pungufu ua kutokulipwa kabisa pia kufanya kazi bila mikataba ya maandishi na kutopata ulinzi wa kijamii.

Pia Ngalo anaeleza kuwa zaidi ya hayo Tanzania haina sheria maalum ambayo inakidhi mahitaji ya wafanayakazi wa nyumbani kwa kuzingatia upekee wa sekta hiyo.Ambapo anaeleza kuwa mfumo wa kisheria wa ajira nchini ni jumuishi kwa wafanyakazi wengine wakiwemo wafanyakazi wa nyumbani.

Sanjari na hayo anaeleza kuwa tofauti na wafanyakazi wengine, wafanyakazi wa nyumbani wameajiriwa katika nyumba binafsi kama mahali pa kazi na hawaonekani kwa umma kwa ujumla hali ambayo inawafanya kutoonekana na kutolindwa ikilinganishwa na wafanyakazi wengine.

“Mara nyingi wanachukuliwa kuwa hawana haki kama wafanyakazi na hivyo hawapewi fursa ya kujadiliana juu ya masharti na matakwa ya kazi wafanyazo ambayo ni pamoja na mambo muhimu kama vile mshahara,saa za kazi na mapumziko,likizo ya mwaka,likizo ya uzazi ,masuala ya afya na usalama wao mahala pa kazi,”anaeleza.

Nini njia ya kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa wafanyakazi wa nyumbani

Ngalo anaeleza kuwa katika kukabiliana na unyanyasaji kwa kundi hilo ambalo ni muhimu katika maendeleo ya taifa ni serikali iridhie Mkataba wa Kimataifa wa Kazi za Staha kwa wafanyakazi wa nyumbani namba 189/2011 na kuweka sheria maalum itakayosimamia ajira ya kazi za nyumbani.

Anaeleza serikali kupitia mamlaka husika itekeleze kikamilifu Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 sambamba na Mkataba wa Shirika la Kazi la Kimataifa(ILO),Na.138/1973 unaoweka katazo la ajira kwa watoto chini ya umri wa miaka 14.

Serikali kupitia mamlaka husika kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya watu wanaoajiri watoto chini ya umri uliowekwa kisheria,kuajiri bila kuwa na mikataba ya maandishi ,kulipa mshahara chini ya kiwango au kutokulipa kabisa.

Pia anaeleza kuwa mamlaka husika za seriakli zisimamia kikamilifu sheria na mifumo ya kupambana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu hususasani kwa watoto.

“Waajiri wa wafanyakazi wa nyumbani wazingatie sheria za ajira ili kuwezesha uwepo wa kazi za staha kwa wafanyakazi wao,wazazi wazingatie wajibu wao katika malezi ili kulinda haki na maslahi ya watoto hususani haki ya kupata elimu,”anaeleza Ngalo na kuongeza kuwa

“Wananchi na wadau wengine waendelee kupaza sauti na kuripoti vitendo vya ukiukwaji wa haki za wafanyakazi wa nyumbani hususani watoto,”.

Sanjari na hayo Ngalo anaeleza kuwa shirika lao la WoteSawa katika kipindi cha kuanzia Januari 2022 mpaka sasa wamefanikiwa kuwaokoa jumla ya wafanyakazi wa nyumbani 165 waliokumbana na ukatili ambapo wamewapa huduma mbalimbali ikiwemo malazi,chakula,msaada wa kisaikolojia,matibabu na msaada wa kisheria.

“Kati ya hao 86 wamerejeshwa na kuunganishwa na familia zao,kwa takwimu hizi ni wazi kuwa ukatili na unyanyasaji kwa wafanyakazi wa nyumbani ni tatizo kubwa na hivyo sote tunapaswa kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na jambo hilo,”anaeleza Ngalo.

Mmoja wa mabinti wafanyakazi wa nyumbani Neema Ishengoma anaiomba serikali kuridhia mkataba wa kimataifa wa kazi za staha kwa wafanyakazi wa nyumbani ambao utasimamia ajira hiyo kwani wanaamini endapo utaanza kufanya kazi utawasaidia wao kuondokana na unyanyasaji hivyo kuwa katika mazingira salama.

Pia amewahimiza waajiri wao kuwapenda na kutowabagua huku jamii iwape kipaumbele kwa kutoa taarifa na kuchukua hatua pindi watoto wafanyakazi wa nyumbani wanapofanyiwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji.

Naye mmoja wa waajiri wa wafanyakazi wa nyumbani Mwalimu Joyce Simon,anaeleza kuwa kundi hilo ni muhimu ambapo ata yeye amelelewa na mfanyakazi wa nyumbani ambaye amechangia mafanikio yake.Hivyo ameiomba jamii kuwatahamini wafanyakazi wa nyumbani ambapo amekua akitoa elimu kwa wanawake wenzie katika vikundi mbalimbali na shuleni juu ya umuhimu wa kundi hilo pamoja na kushirikiana na uongozi wa mtaa kuwachukulia hatua baadhi ya waajiri ambao wamekua wakiwafanyia ukatili wafanyakazi wao wa nyumbani.

Kwa upande wake Ofisa Kazi Mkoa wa Mwanza Betty Mtega kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,anaeleza kuwa waajiri wa wafanyakazi wa nyumbani wanapaswa kusaini mikataba ya maandishi yenye viwango vya mishahara vilivoidhinishwa na sheria.

Kauli mbiu ya siku ya kimataifa ya Mfanyakazi wa Nyumbani inasema ‘Hakuna usawa wa kijamii bila kuwa na kazi za staha kwa wafanayakazi wa nyumbani’,kwa mujibu wa kauli mbiu hii waajiri wanaaswa kuwalipa wafanyakazi wao wa nyumbani kwa kuzingatia kima cha chini cha mshahara kama ilivyoainishwa katika amri ya kima cha chini cha mshahara tangazo la serikali Na.687/2022,”anaeleza Mtega na kuongeza kuwa

“Iliyoanza kutumika Januari Mosi mwaka huu ambayo ni shilingi 60,000 kwa wafanayakazi wa nyumbani wanaoishi katika kaya ya mwajiri na 120000,kwa wasioishi katika kaya ya mwajiri na 200000 kwa walioajiriwa na maofisa wenye stahiki na 250000 walioajiriwa na wanadiplomasia au wafanyabiashara wakubwa,”.

Sanjari na hayo anaeleza kuwa ni kosa kisheria kumuajiri mtoto mwenye umri chini ya miaka 14 hivyo ameitaka jamii kuungana kwa pamoja kupinga ajira kwa watoto au kuwafanyisha watoto kazi zozote zinazowazuia kuendelea na masomo na kuzuia maendeleo chanya.

“Nina uhakika kuwa mnafahamu kabisa suala la ajira kwa watoto wapo watu ambao huwaajiri watoto kufanya kazi za nyumbani chini ya umri,nawaasa tuepuke kuwaajiri watoto chini ya umri,”anaeleza Mtega na kuongeza kuwa

“Ni vyema kuwahimiza watoto wetu kuweka jitihada zao katika elimu kwani ndio msingi wa maisha na ndio taifa la kesho,serikali kupitia mamalaka husika itawachukulia hatua za kisheria watu watakaobainika kuwaajiri watoto chini ya umri,”.

Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza Gigwa Masanja,anaeleza kuwa wamekuwa wakiwaokoa wafanyakazi wa nyumbani kwa kushirikiana na wadau na wengi wanao wapokea unakuta wamefanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kupingwa,kuchomwa na moto au kitu chenye ncha kali na kulazimishwa kufanya mapenzi na waajiri wao.

“Kama binti unafanya kazi za nyumbani ukiwa na malengo hivyo usiruhusu vitendo kama hivi kuharibu ndoto zako pia dawa ya moto ni nini? mwajiri akikufanyia ukatili usilipize kwa mtoto bali toa taarifa ili waweze kuchukulia hatua na serikali imerahisisha unapofanyiwa ukatili toa taarifa kwa kupiga simu namaba 116, hivyo Ofisa Ustawi ambao wapo karibu watapigiwa simu na kufika eneo husika na hatua zitachukuliwa,”.

Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza Charlse Keah,ametoa wito kwa jamii kuwajali wafanyakazi wa nyumbani kuwapenda,kuwajenga,wawahudumia na wawape stahiki zao halali na endapo wakiumwa wawapeleke hospitali kwa ajili ya matibabu pamoja na kuwapa likizo kwasababu ni watu muhimu katika jamii.

Pia amewahimiza wazazi kuwafundisha watoto wao kufanya kazi ndogo ndogo za nyumbani hasa kipindi cha likizo kulingana na umri na siyo kazi zote aachiwe dada wa kazi.

“Kwani ndio tunawaacha nyumbani wanatuangalizia watoto wetu natoa wito kwa jamii na tutaendelea kuelimisha umuhimu wa wafanyakazi wa nyumbani ambao mkiwafanyia ukatili hawawezi kuwalipizia nyie kwa vile mnawazidi nguvu lakini watakachofanya watalipiza kwa watoto wetu hivyo tuishi nao vizuri kama watoto wetu na wenyewe watatuthamini na familia itakuwa na amani,upendo na salama,”.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi kwa niaba ya Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mwanza Fortunata Scandor,anaeleza kuwa katiba ya nchi inasema watu wote wana haki sawa kila mtu ana haki ya kuishi na kupata haki zote.

Fortunata anaeleza kuwa wafanayakazi wa nyumbani wanapaswa kutambua kuwa kazi hiyo siyo ya laana bali kila mtu ana karama ambayo alipewa na Mungu na kila mtu amepewa jukumu lake tofauti mwingine atakuwa kiongozi,mfanyakazi wa nyumbani na kadhalika.

Anaeleza kuwa haki inaendana na wajibu hivyo wafanyakazi wa nyumbani watimize wajibu wao kwa waajiri wao huku akiwasisitiza kuwa pale wanapoona haki zao za msingi zinavunjwa wasikae kimya kwani serikali ipo wapaze sauti kupata msaada.

“Tufichue uharifu inawezekana katika kufanya kwetu kazi za nyumbani kuna uhalifu unatendeka wasikae kimya kama umetendewa vitendo vya ukatili au kuna viashiria kama kubakwa msikae kimya,kukaa kimya kunaweza kusababisha ukapata madhara mfano ukipata mimba waajiri wanawafukuza na kurudi kijijini ambapo umaskini hauwezi kuisha,”anaeleza.