March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yataka wananchi wajiunge na NHIF kwa uhakika wa matibabu


Na Joyce Kasiki, Timesmsjira Online ,Mbeya

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameuagiza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuendelea na jitihada za kuhamasisha wananchi kujiunga na huduma ya bima ya afya, ili wawe na uhakika wa kupata matibabu kabla ya kuugua.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo, Oktoba 10, 2025, jijini Mbeya alipokuwa akitembelea banda la NHIF katika maadhimisho ya Wiki ya Vijana yanayofanyika mkoani humo.

Amesema kuwa sekta ya afya ni nguzo muhimu katika maendeleo ya Taifa, na ndio maana Serikali imeanzisha mpango wa bima ya afya kwa wote, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu bila vikwazo vya kiuchumi.

“Ni muhimu kuendelea kuhamasisha makundi mbalimbali ya jamii, ikiwemo vijana, waendesha bodaboda, bajaji, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla, ili waone umuhimu wa kujiunga na bima ya afya.”amesisitiza

Kwa upande wake, Meneja wa NHIF Mkoa wa Mbeya, Dkt. Eliud Kilimba, amemueleza Waziri Mkuu kuwa ushiriki wao katika maonesho hayo unalenga kutoa elimu kwa vijana na wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na NHIF.

โ€œTupo hapa kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu huduma zinazotolewa na NHIF, ili kuwahamasisha wananchi kujiunga na mfumo huu ambao utawawezesha kupata matibabu kwa uhakika kabla hawajaugua,โ€ amesema Dkt. Kilimba.

Ameongeza kuwa, kwa wale wanaoonyesha utayari wa kujiunga, wanapatiwa maelekezo ya moja kwa moja kuhusu hatua za usajili hapo hapo uwanjani.