November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baadhi ya maduka, sukari imepanda bei kama inavyoonekana pichani (Picha ya Mtandao)

Serikali yataja sababu sukari kuongezeka bei

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

SERIKALI imewahakikishia Watanzania kuwa hakuna upungufu wa sukari nchini, hivyo wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi wa aina yoyote ile, huku ikisema hali hiyo imesababishwa na waagizaji kushindwa kuagiza kwa wakati kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na kirusi cha Corona

Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, ameyasema hayo
Jijini Dodoma leo wakati akitoa ufafanuzi juu ya malalamiko ya
wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya sukari.

Amesema kuwa kila mwaka Serikali imekuwa makini katika kutathmini
mahitaji ya sukari kwa wananchi pamoja na uwezo wa viwanda vya ndani katika uzalishaji.

Bashungwa amesema; “Ni kweli bei ya sukari imepanda, lakini
haisababishwi na upungufu wa sukari, bali imesababishwa na waagizaji
kushindwa kuagiza kwa wakati kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na kirusi cha Corona.”

Ili kukabiliana na kadhia hiyo, alisema Serikali imetoa vibali vya
jumla ya tani 40,000 kwa kampuni nne za wazalishaji ambapo kila
kampuni imeagiza tani 10,000

Waziri Bashungwa alisema kuwa tayari sukari iliyokwisha ingia
bandarini kupitia kampuni ya Kagera Sugar ni tani 9,990 na imeanza
kutolewa bandarini tangu jana jioni.

Kadhalika alisema Aprili 24, 28 na 30 kampuni ya Mtibwa Sugar
itaingiza jumla ya tani 10,000. Kampuni ya Kilombero Sugar itaingiza
jumla tani 1,624 hivi karibuni kutoka Malawi na Msumbiji, huku tani
1,800 zikiagizwa kutoka Afrika Kusini.

Sambamba na hayo alisema kuwa wiki ya kwanza ya Mei  Kampuni ya
Kilombero Sugar itaingiza tani 7,276 huku tarehe 15 Mei kampuni ya TPC itaingiza Tani 5,000 na Tarehe 30 Mei Tani 4,500 zitaingia nchini.

Katika hatua nyingine Waziri Bashungwa alisema kuwa Wizara inatarajia kuomba nyongeza ya tani 58,000 ili kukidhi mahitaji ya sukari kufikia Juni 2020

Alisema kwa mujibu wa takwimu mahitaji ya sukari inayotumiwa majumbani ni kiasi cha tani 4,700,000 ambapo kati ya hizo, tani 378,000 zinazalishwa nchini.

Bashungwa alisema hiyo ni hatua kubwa kwa nchi na serikali katika
mkakati wa kuimarisha uchumi wa viwanda huku wawekezaji wengi
wakiendelea na mchakato wa uongezaji tija na uwezo wa uzalishaji

Alisema wakulima wamekuwa na mtazamo mkubwa katika kuzalisha miwa kwa wingi ambayo wataipeleka katika viwanda vya kuchakata sukari na katika kipindi cha hivi karibuni ambapo serikali itafikia uwezo mkubwa wa uzalishaji hivyo kuwa na ziada ya sukari itakayouzwa nje ya nchi.