February 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yashirikiana na wananchi kujenga shule karibu na makazi Musoma vijijini

Fresha Kinasa, TimesMajira Online Mara.

SERIKALI kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini,Prof.Sospeter Muhongo pamoja na Wananchi kwa pamoja wameendelea kuimarisha sekta ya Elimu katika jimbo hilo ili kuhakikisha shule za Sekondari  zinakuwa karibu kuwapa fursa nzuri Watoto kusoma karibu na Makazi yao.

Hayo yamesemwa  kupitia Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo Prof. Muhongo  Februari 18, 2025, ambapo pamoja na mambo mengine imebainisha kuwa, hivi sasa Sekondari 12 zinajengwa jimboni humo ili kila mtoto apate fursa ya elimu kwa urahisi kwa faida ya maisha yake,Jamii na Taifa pia.

Taarifa hiyo imesema,Kati ya Sekondari hizo 12 zinazojengwa,Sekondari tatu zinajengwa na Serikali kuu,huku  Sekondari tisa zikijengwa kwa kutumia nguvu kazi na michango ya fedha kutoka kwa Wanavijiji, Wazaliwa wa Vijiji vyenye ujenzi na viongozi wao.

“Sekondari tatu, zinazojengwa na Serikali kuu ujenzi kukamilika Februari 28, 2025, ni  Kijijini Butata kata ya Bukima,  Kijijini Kasoma, Kata ya Nyamrandirira na Kijijini Kurwaki kata ya Mugango. Na pia  Wanavijiji wamekubali kuchangia nguvu kazi zao kwenye ujenzi wa Sekondari hizo.” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa,Sekondari tisa zinajengwa kwa kutumia nguvukazi na michango ya fedha kutoka kwa wanavijiji, wazaliwa wa vijiji vyenye ujenzi na viongozi wao ni katika  Kijiji cha Muhoji, Kata ya Bugwema itafunguliwa Februari 28, 2025. Pia zingine ni katika
Kisiwa cha Rukuba, Kata ya Etaro na
Kijiji cha Mmahare, Kata ya Etaro.

“Pia Kijiji cha Nyasaungu, Kata ya Ifulifu, Kijiji cha Kiriba, Kata ya Kiriba,Kijiji cha Kataryo, Kata ya Tegeruka,Kijiji cha Musanja, Kata ya Musanja,Kijiji cha Chitare, Kata ya Makojo na Kijiji cha Nyambono, Kata ya Nyambono.”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha Prof.Muhongo ametoa rai kwa Wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo Wananchi jimboni humo na Mkoa wa Mara kwa ujumla kuunga mkono ujenzi wa shule Mpya  za Sekondari unaoendelea jimboni humo pamoja na ujenzi wa shule za Msingi katika kuandaa Wasomi watakaoleta tija kwa Taifa na Jamii katika nyaja za Maendeleo ya kiuchumi na Kijamii.

Rhoda Paulo ni Mkazi wa Kata ya Nyakatende katika Jimbo la Musoma Vijijini ameiambia Majira Online kuwa ” Watoto wakisoma karibu na nyumbani ufanisi utaongezeka kitaaluma,  badala ya kutembea umbali mrefu, Watoto watatembea  umbali mfupi tena kwa muda mchache kufika  shuleni. Naishukuru Serikali, Mbunge wetu na Wananchi wenzangu  tumeendele kushikamana kuchangia maendeleo bila kurudi nyuma kwa faida yetu chini ya usimamizi makini wa Prof. Muhongo. ” amesema Rhoda.

Jimbo la Musoma Vijijini lenye jumla ya Kata 21,  lina Sekondari 26 za Kata/Serikali  na Sekondari 2 za Madhehebu ya Dini.