Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Tunduma.
SERIKALI imeendelea na juhudi zake za kuboresha huduma za maji kwa wananchi, baada ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Tunduma-Vwawa wenye thamani ya shilingi bilioni 119.9
Mkataba huo umesainiwa kwenye hafla iliyofanyika katika viwanja vya mwaka kati, mjini Tunduma na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Maji, Juma Aweso na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Akitoa taarifa ya Mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, alisema kuwa mradi huo
utatekelezwa na Mkandarasi kutoka kampuni ya CCECC ya China kwa fedha kutoka serikali ya Tanzania.
Amesema utahusisha ujenzi wa chanzo cha maji (intake) kwenye Mto Momba, kituo cha kuchakata na kutibia maji (Treatment Plant), mtandao wa mabomba ya kusambaza maji, matenki ya kuhifadhi maji, pamoja na ununuzi na ufungaji wa pampu za maji.
Aidha amesema chanzo hicho kitakuwa na uwezo wa kuchukua maji lita 21,506,000 kwa siku, na kituo cha kuchakata maji kitaweza kuzalisha lita 20,000,000 kwa siku.
Vilevile, ujenzi wa mtandao wa mabomba utahusisha mabomba yenye kipenyo cha kati ya 100mm hadi 600mm, na matenki yatakayohifadhi lita 5,000,000 – Uwanjani/Uhuru, lita 3,000,000 – Ikana na lita 2,000,000 – Nkangamo.
Pia,amesema mradi huo utahusisha ujenzi wa ofisi kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi wa mradi, na ununuzi wa vitendea kazi mbalimbali.
Akizungumza baada ya utiaji saini, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, alisema kuwa utekelezaji wa mradi huu ni sehemu ya ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa mkoa wa Songwe.
Amesisitiza kuwa mradi huo utakuwa chachu ya maendeleo kwa mki wa Tunduma katika Wilaya ya Momba na mji wa Vwawa katika Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Aweso, alizungumzia umuhimu wa mradi kwa wananchi wa Tunduma, akisema kuwa mradi huu utatatua changamoto kubwa ya maji katika mji wa Tunduma.
Amempongeza Mbunge wa Tunduma, Silinde, kwa juhudi zake katika kushinikiza utekelezaji wa mradi huu, akisema kuwa ni vigumu kupata viongozi wanaojitolea kwa dhati kuleta maendeleo.
Aweso pia alimtaka mkandarasi kufanya kazi kwa kuzingatia mkataba na alionya kuwa atawajibika endapo atachelewesha utekelezaji.
Naye,Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elias Mwandobo,amefafanua kuwa upatikanaji wa maji katika mji wa Tunduma ni asilimia 45.2, na mradi huu utakuwa muarobaini wa tatizo hilo, kwani utahakikisha kuwa mji huo unapata huduma ya maji kwa wingi na ubora.
Aweso amesema kuwa Mradi huo awali ulipangwa kutekelezwa kwa fedha za wafadhili wa nje, lakini baada ya ushauri wa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, sasa utatekelezwa kwa fedha za ndani, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kudhibiti utegemezi wa nje na kuimarisha uchumi wa ndani.
Kwa upande wa Silinde,ameeleza shukrani zake kwa Serikali ya Rais Samia, akisema kuwa mradi huu utaboresha maisha ya wananchi wa Tunduma na kusaidia kuondoa changamoto za maji kwa wananchi wa Tunduma na maeneo ya jirani.


More Stories
Kamati ya kudumu ya Bunge yapongeza ujenzi wa jengo la Wizara ya Nishati Mtumba
Gawio kutoka kampuni ambazo Serikali ina hisa chache zapaa kwa asilimia 236
Pinda:Vijana tumieni fursa kupata maarifa ya ufundi stadi