Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya ALAMEDA kutoka MISRI wamesaini makubaliano yatayotoa fursa kwa Wataalamu wa afya kutoka Tanzania kupata mafunzo ya huduma bobezi zakibingwa kutoka kwa Wataalamu wa Hospitali hiyo ya Misri, jambo litalonufaisha Watanzania kwa huduma hizo.
Prof. Makubi ameyasema hayo, leo Oktoba 20, 2022 katika tukio la kusaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano pamoja na Mtendaji Mkuu wa Alameda Healthcare Group kutoka nchi ya Misri Bw. Neeraj Mishra ikiwa ni sehemu ya kuboresha ushirikiano wa kimataifa baina ya nchi hizo, tukio lililofanyika katika ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma.
“Leo Oktoba 20, 2022 tumesaini makubaliano ya pamoja yatayosaidia kuboresha huduma ikiwemo kunufaika kwa watalaamu zaidi ya 20 kila mwaka kutokana na mafunzo kwa watumishi wa afya katika nyanja za ubingwa na ubingwa bobezi watayoendelea kupata kutoka kwa Wataalamu wa nchi ya Misri.” Amesema Prof. Makubi.
Ameendelea kusema kuwa, Ushirikiano baina ya nchi ya Tanzania na Misri unatokana na mizizi ya uhusiano mzuri uliowekwa na viongozi wa nchi hizo, hivyo Wizara ya Afya itaendelea kuimarisha ushirikiano huo ili kuhakikisha Wananchi wanapata huduma za Afya bora na kwa gharama nafuu kwa wote.
Aidha, Prof. Makubi amesema kuwa, Mkataba uliosainiwa leo kati ya nchi ya Tanzania na Hospitali ya ALAMEDA kutoka MISRI ni wa saba, huku akisisitiza kuwa, hati hii ya makubaliano imelenga kuimarisha utoaji huduma za afya kwa Wananchi kwa gharama nafuu.
Sambamba na hilo, amesema kuwa, hati za makubaliano zingine zilizosainiwa zimelenga kuimarisha mashirikiano ya kikanda katika masuala ya udhibiti wa magonjwa ya dharura mipakani ili kuzuia kusambaa kwa magonjwa hayo.
Pia, Prof. Makubi amesema kuwa, makubaliano haya yamelenga katika kuhamasisha masuala ya tafiti za tiba na kinga ili kuibua changamoto mbalimbali katika jamii na kuzitafutia suluhu ili kuikinga jamii dhidi ya magonjwa hayo. Hata hivyo, Prof. Makubi amesema, mashirikiano hayo yatasaidia kuimarisha huduma za tiba mtandao na mifumo ya TEHAMA katika maeneo ya utendaji, hali itayosaidia kuimarisha upatikanaji wa takwimu sahihi na kuongeza ufanisi katika kufanya maamuzi sahihi katika ngazi ya utendaji.
Ameongeza kuwa, katika kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini, Serikali inaendelea kushirikiana na Wadau katika uwekezaji wa tiba na viwanda vya dawa na vifaa tiba ili kupunguza Rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa matibu na kuokoa fedha ambazo zingetumika kwa matumizi hayo.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya ALAMEDA kutoka nchi ya MISRI, amesema Hospitali yao ina zaidi ya vitanda 1000, huku akiweka wazi ushirikiano mkubwa wanaopata kutoka kwa Serikali yao katika kuboresha huduma kwa wananchi.
Kwa upande mwingine Bw. Neeraj Mishra ameweka wazi kuwa, moja ya sababu ya kufanikiwa kwa nchi ya Misri katika Sekta ya afya ni kuingia katika mfumo wa Bima ya afya kwa wote unaotoa fursa kwa wananchi wao kupata huduma bora za afya na zenye gharama nafuu wakati wote.
More Stories
Kapinga asema mafanikio katika sekta ya nishati yanatokana na jitihada za Rais Samia
Bumbuli kutekeleza miradi kwa kuangalia vipaumbele
Makalla:Kupanga fujo ni dalili za kushindwa uchaguzi