Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto
Serikali imeendelea kupunguza changamoto katika sekta ya elimu katika Halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga kwa kutoa fedha kwa ajili ya miundombinu ikiwemo vyumba vya madarasa na nyumba za walimu.
Hayo yamesemwa Februari 21, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro kwenye kikao cha tathmini ya elimu kwa Halmashauri ya Bumbuli kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.
Ambapo kulikwenda sambamba na kuwapa zawadi ya fedha taslimu kama motisha kwa walimu, shule na kata zilizofanya vizuri kwenye mitihani ya darasa la saba na la nne mwaka 2023.
Lazaro amesema moja ya changamoto kwenye sekta ya elimu ni upungufu wa miundombinu muhimu ya shule ikiwemo vyumba vya madarasa, lakini wengi ni mashahidi wa miradi ya ujenzi inayoendelea, na kiasi cha fedha kilichotolewa kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Amesema serikali ilitoa kiasi cha milioni 475 kupitia ruzuku ya Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu, ukamilishaj na ujenzi wa vyumba vya madarasa,pia kupitia mpango wa EP4R ilitoa kiasi cha milioni 40.
Kupitia mradi wa BOOST, Serikali ilitoa kiasi cha milioni 937 zilizotumika kujenga shule mpya ya mkondo mmoja, madarasa na matundu ya vyoo katika shule sita za msingi.
“Serikali ilitoa kiasi cha milioni 77.8 kupitia mradi wa GPE LANES II kukarabati kituo cha Walimu na kujenga vyumba vya madarasa na miradi mingine mingi iliyokamilika na inayoendelea kujengwa, hizi zikiwa ni jitihada za Rais Dkt. Samia kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata elimu bora katika mazingira bora,” amesema Lazaro.
Lazaro amesema jitihada za walimu zinatambulika na zinathaminiwa na amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli Baraka Zikatimu kwa kuthamini mchango wa walimu katika matokeo hayo mazuri ya kitaaluma na kuweza kuwapa zawadi ya fedha taslimu.
“Motisha ni mbinu mojawapo ya kuongeza jitihada na kuleta ufanisi, hivyo nampongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli kwa kuthamini mchango wa walimu katika matokeo mazuri ya kitaaluma” amesema Lazaro.
Lazaro aliwasihi walimu mambo manne ikiwemo kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi ambacho kitaboresha pamoja na mambo mengine, kitaongeza mahudhurio ya wanafunzi shuleni.
Pia, uwajibikaji kwa kila mwalimu katika vituo vya kazi, kuepuka mikopo inayokiuka viwango vya riba vilivyopendekezwa na usimamizi mzuri wa miradi inayopelekwa katika shule zao.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli, Baraka Zikatimu, amesema zawadi ikiwemo fedha taslimu walizotoa kwa walimu ni mwanzo tu.
Lakini mwaka huu wataongeza zawadi zaidi ili kuona wanawapa motisha walimu ili wafanye vizuri zaidi katika kuwapa taaluma wanafunzi.
“Kwenye mtihani wa darasa la saba mwaka huu (2024), shule itakayoweza kuwafanya wanafunzi wafaulu kwa alama asilimia 80, walimu watapata sh. 500,000, asilimia 85 sh. 600,000, asilimia 90 sh. 700,000, asilimia 95 sh. 800,000 na asilimia 100, Mwalimu Mkuu aje achukue sh. milioni 1,000,000 akagawane na walimu wenzake” amesema Zikatimu.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bumbuli Ameir Sheiza, amegawa mitungi ya gesi 99 kwa ajili ya shule za msingi 99 kati ya shule 100 za halmashauri hiyo.
Majiko hayo ni kwa ajili ya walimu kujipikia chakula kwenye shule zao na yametolewa kama msaada na Mbunge wa Jimbo la Bumbuli January Makamba.
More Stories
Mwanasheria Mkuu apiga kura uchaguzi wa serikali za mitaa
CHADEMA yasikitishwa mawakala wao kuzuiliwa
Rais Samia amlilia Dkt. Ndugulile