November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yapongeza vijana kuchangamkia fursa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online- Zanzibar

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amelipongeza Baraza la Vijana Kibweni kwa kutumia fursa zilizopo nchini kupitia nyanja mbalimbali zikiwemo ushonaji na taasisi za kifedha ili kujiletea maendeleo na kukuza uchumi wa Taifa.

Naibu Waziri Katambi aliyasema hayo Machi 09,2022 wakati Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ilipofanya ziara ya kutembelea na kuona shughuli zinazofanywa na vijana Zanzibar akisema hatua hiyo inaonyesha uthubutu wa vijana kupambana na changamoto ya ajira.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inaweka miundo mbinu rafiki kwa vijana kuanzisha viwanda vidogo vidogo na kujiajiri katika ujasiriamali.

“Nimefurahi sana kupata nafasi ya kutembelea hapa na kuona shughuli mnazozifanya kama Fuoni na kibondeni kujionea kilimo cha kisasa (Kitalu Nyumba) na kituo cha Radio Kati Fm ambayo ni ya kijamii ya Baraza la Vijana na kiwanda cha ushonaji, yapo ambayo tumejifunza na mengine sisi kama Serikali tunayachukua hasa suala la uwekezaji kwa vikundi, malezi na mafunzo,” alisema Mhe. Katambi.

Vile vile alitaja shughuli zingine zinazofanywa na baraza hilo kuwa ni ushonaji, masuala ya taasisi za kibenki kwa mifumo ya Simu pamoja na uchomeleaji akisema uamuzi huo unainyesha vijana wako tayari kufanya kazi huku akisisitiza kuendelea kujifunza na kuwa wabunifu kuleta ustawi kwa vijana wa Tanzania Bara na Visiwani.

Katika hatua nyingine Mhe. Katambi alieleza kwamba serikali itaendelea kutatua changamoto ya masoko kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini na vijana zinapata masoko ya ndani na nje ya Nchi na kuweka kutenga maeneo sahihi kwa ajili ya vijana kufanya biashara zao.

“Nitoe wito kwa Wizara wizara kuangalia changamoto ya masoko ya bidhaa zinazozalishwa na vijana hawa jambo ambalo ni la Kiserikali na tumelichukua tunalifanyia kazi, pia kuna maeneo mengine tunatakiwa kuyatenga sababu maeneo mengi ya vijana ambayo tumeyazungukia wana Changamoto zinazofanana kwa upande wa Tanzania Bara na Visiwani ,”alifafanua .

Kwaupande wake Katibu Mkuu Wizara ya , Habari ,Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Rajabu alibainisha kwamba wako tayari kutoa ushirikiano katika mabaraza la vijana ili wajikwamue kiuchumi huku akiishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu na Kamati hiyo kwa kuwatembelea hatua inayowatia moyo vijana kusonga mbele.

Aidha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Dkt. Joseph Mhagama alisema kutokana na yale waliyoyabaini kufuatia ziara hiyo sekretarieti itayafanyia kazi na kupongeza utayari wa vijana kujifunza na kuwajengea uwezo.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anaye shughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipotembelea maeneo mbalimbali Machi 09, 2022 Visiwani Zanzibar.
Katibu Mtendaji Baraza la Vijana Zanzibar Bw. Salum Ameir (wa kwanza kushoto) akitoa maelezo kuhusu eneo la vijana wanaojishughulisha na kilimo cha kisasa (Kitalu Nyumba) katika ziara ya Kamati hiyo.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi pamoja na wajumbe wa Kamati ya Budumu ya bunge ya Katiba na Sheria walipotembelea kikundi cha Kibweni cha masuala ya taasisi za kifedha kupitia mifumo ya simu.
Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Dkt. Joseph Mhagama ( wa pili kushoto), Mwenyekiti Msaidizi Bi. Najima Giga ( wa kwanza kushoto) na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi (wa pili kulia) na Mkurugenzi Msaidizi wa Kituo cha Redio Jamii ya Baraza la Vijana (Kati Fm), (wa kwanza kulia) wakizungumza jambo walipo tembelea Redio hiyo.
Viongozi mbalimbali kutoka Tanzania bara na Visiwani pamoja na wajumbe kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakiwa katika picha ya pamoja katika ziara iliyofanyika Zanzibar Machi 09, 2022.