January 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TBS yapongezwa kutafsiri maono ya Rais

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Dar

SERIKALI imesema hatua ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kupatiwa Cheti cha Umahiri wa Kutoa Huduma ya Ithibati Ubora wa Bidhaa inadhihirisha jinsi shirika hilo lilivyotafsiri kwa vitendo maono na miongozo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Kauli hiyo ilitolewa Ijumaa na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, kwenye hafla ya kukabidhi TBS Cheti cha Umahiri wa Kutoa Huduma ya Ithibati Ubora wa Bidhaa kutoka SADCAS jijini Dae es Salaam.

Dkt. Abdalllah ameongeza kuwa hatua hiyo inadhihirisha umma kuwa kauli ya Rais Samia ya kuwa sasa tuko tayari kuingia kwenye masoko ya kimataifa tukiwa na bidhaa bora, TBS imeweza kukamilisha ndoto hiyo.

Amefafanua kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia imedhamiria kujenga misingi shindani na endelevu ambayo haiwezi kupatikana kama bidhaa si bora.

“Mnavyopata cheti kutoka SADCAS maana yake mmefaulu ndani ya jumuiya ya kimataifa kwamba mnao uwezo wa kuthibitisha ubora wa bidhaa, kwa hiyo kampuni zetu ndani ya nchi, wafanyabiashara wetu ndani ya nchi watakuwa na uhakika kwamba bidhaa zinazothibitishwa na TBS ni bora katika soko la kimataifa,” amesema Dkt. Abdallah.

Ameongeza kusema kuwa Serikali inayoongoza na Rais Samia itaendelea kuimarisha mahusiano na taasisi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kupata ufadhili katika kuendesha taasisi hizo za udhibiti ubora .

“Aidha, kupitia jitihada hizi Serikali ilifanikiwa kupata ufadhili wa Trademark Afrika ambapo wafadhili waliwajengea uwezo watumishi wa TBS kuwa na umahiri unaohitajika kwa mujibu wa kiwango ca kimataifa,” amesema na kusisitiza kwamba;

“Hili jambo kwa hakika ni zuri na la kupongezwa kwa Serikali yetu kwa kuwa na wadau muhimu ambao wanaunga mkono jitihada zetu za kuimarisha mifumo ya usimamizi wa ubora wa bidhaa.”

Amesema mafanikio hayo yanawapeleka katika hatua nyingine ya mafanikio ya uchumi wa nchi yetu, kwani Tanzania imeingia kwenye eneo Huru la Biashara Afrika, soko ambalo linahitaji sana bidhaa na huduma zilizo bora, hivyo ubora ni mojawapo ya kigezo cha kulifikia soko hilo na masoko mengine kikamilifu.

“Kwa muktadha huo Tanzania tumeingia kwenye soko hili kubwa kifua mbele tukiwa tumewezeshwa na si mwingine bali TBS kuvuka vikwazo vya ubora wa bidhaa, niwaombe wafanyabiashara na wazalishaji nchini tuitumie TBS kuhakikisha tunauza bidhaa zenye kukidhi viwango na shindani sokoni,” amesema Dkt. Abdallah na kuogeza;

“Cheti hiki cha umahiri kinakuwa ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa biashara Afrika, hasa zile zinazovuka mipaka ya Tanzania zilizothibitishwa ubora na TBS hazitapata vikwazo vya kiufundi tena kwenye mipaka ya nchi zinazofanya nazo biashara.”

Amewashukuru wazalishaji hasa walioingia kwenye mchakato huo, kwani bidhaa zilizoingia kwenye mchakato huo zimeweka wigo mpana wa Ithibati mahiri kwa kuwapa ushirikiano wa hali ya juu, kuruhusu TBS kufanya ukaguzi na kuhakiki katika zile bidhaa zilizowahusisha wakaguzi wa SADCAS.

“Ushirikiano mkubwa kwenye shughuli hii inadhihirisha ni mashirikiano makubwa mlinao sio tu ndani ya TBS, ndani ya wizara, lakini mnaunga mkono juhuhi za Rais Samia,” alisema.

Ameishukuru SADCAS kwa kukubali ombi la TBS la kufanyiwa tathmini ya umahiri ambayo imepelekea kupatikana kwa Ithibati hiyo.

Kwa niaba ya Serikali sisi Wizara ya Viwanda na Biashara tutaendelea kusimamia, kufuatilia na kuhakikisha kuwa Ithibati hiyo inaendelea kulindwa kwa TBS kuzingatia matakwa yote yaliyoainishwa na SADCAS.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amesema maabara zote tisa za TBS zimeishathibitishwa mifumo na zina Ithibati.

“Lakini pia tumepata Ithibiti ya umahiri katika mifumo ya usimamizi wa viwango kimataifa na TBS inatoa huduma hiyo hapa nchini na mifumo hiyo viwanda na taasisi mbalimbali tayari zimeishathibitishwa,” amesema Dkt. Katunzi.

Aidha, Dkt. Katunzi amesema kutokana na kuhimarika kwa uhuduma za shirika, mifumo yake ya udhibiti wa ubora imekuwa ikipokea maombi ya viwanda kutoka nje ili kuweza kuthibitisha ubora wa bidhaa zao.

Alisema hadi sasa wana takribani bidhaa 87 zinazozalishwa huko duniani ambazo zimethibitishwa ubora wake na TBS na kuweza kutumia nembo ya shirika ya ubora ili bidhaa zake ziweze kutumika hapa nchini.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa SADCAS Christine Gadzikwa, ameipongeza TBS kwa hatua kubwa ambayo imefikia, kwani hatua hiyo sio kazi rahisi.