Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM
SERIKALI imewahamasisha vijana kujiunga na program atamizi inayotolewa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), ili wapate ujuzi wa biashara na hatimaye kuwa wafanyabiashara wazuri wanapomaliza elimu ya vyuo.
Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Sempeho Manongi, wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa siku ya atamizi.
Uzinduzi huo uliofanywa kwenye chuo cha CBE ulifanywa na Afisa Tawala wa Mkoa wa Ilala, Charangwa Selemani na unalenga kuwawezesha wanafunzi wenye mawazo ya biashara kuyakuza na hatimaye kuwa wafanyabiashara wakubwa.
Amepongeza hatua ya chuo hicho kuanzisha program hiyo akisema kwamba inaleta uhalisia zaidi kuliko masomo ya nadharia na itawasaidia sana wanafunzi wa chuo hicho kupata ujuzi wa biashara.
“Nafuraji kuona chuo cha elimu ya biashara kimesimama kwenye misingi ya kuanzishwa kwake kwa kuanzisha progamu kama hii ya atamizi ambazo zitakuwa na matokeo ya haraka sana kuliko nadharia, mnatakiwa kuishi kwenye maisha ya watu ya sasa ili waweze kujiajiri na kwa hili mnafanikiwa” amesema
“Natamani mboreshe zaidi ili vijana wengi wanaomaliza hapa CBE wawe wameshapata elimu ya ujasiriamali kama hii ambao sasa wataajiri vijana wengine wanaotoka kwenye vyuo mbalimbali,” amesema Manongi
Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Tandi Edda Lwoga, amesema CBE iliamua kuanzisha program hiyo atamizi ya biashara ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan na kimeendelea kuweka mipango mbalimbali madhubuti kuinua ubora wa chuo.
“Sisi CBE tumaanini hizi program atamizi za biashara na teknolojia zitachangia kuibua na kulea ndoto za biashara za wanafunzi ili hata wakimaliza vyuo waendeleze biashara zao na kuajiri wengine,” amesema Lwoga
Amesema chuo hicho kilianza program atamizi mwaka juzi na mwaka jana walianza msimu wa kwanza wanafunzi 100 kwenye progamu hiyo na wengine wameshiriki kwenye maonyesho kuonyesha walivyofanikiwa kwenye kujiajiri wakiendelea na masomo.
Amesema chuo hicho kimewekeza kwenye atamizi ya biashara ili kuionyesha dunia kwamba wanatoa mafunzo kwa vitendo ili kupunguza tatizo la ajira nchini kwa wanafunzi wanaomaliza kujiajiri wenyewe.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria