December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi wa Knight Support, Blessing Kachambwa na wenzake wahasibu wawili wakiwa chini ya ulinzi wakipelekwa kituo cha Polisi walipokamatwa Makao Makuu ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) baada ya kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wa Knight Support. Na Mpigapicha Wetu.

Serikali yaonya vikali waajiri wasiowasilisha michango NSSF

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

SERIKALI imetoa onyo kali kwa waajiri wote nchini, wanaokata michango ya wafanyakazi, lakini hawaiwasilishi kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ukiwemo Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuwa kufanya hivyo ni sawa na wizi mwingine au uhujumu uchumi.

Serikali imesema kuanzia sasa itawachukulia hatua kali za kisheria waajiri wa aina hiyo ambao hawazingatii matakwa ya kisheria na kwamba kuanzia sasa itafanya operesheni kubwa ya kuwasaka waajiri wa aina hiyo na kuwachukulia hatua stahiki.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde alipokutana na Menejimenti ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na uongozi wa Kampuni ya Ulinzi ya Knight Support ambao haujawasilisha michango ya wafanyakazi wake kwa takribani miaka 10.

Amesema kumekuwepo na kesi ya muda mrefu ya wafanyakazi wa Knight Support ambapo tayari NSSF ilichukua hatua za awali baada ya madai ya muda mrefu ya wafanyakazi wakawapeleka mahakamani.

Mavunde amesema Mahakama ili itoa hukumu na ilipaswa kwenda kukaza hukumu kwa ajili ya kukamata mali za mwajiri ili waweze kufidia michango ambayo haijawasilishwa jumla ya sh. Bilioni 8.417 inayojumuisha michango na tozo za adhabu.

Amesema wahusika wa kampuni hiyo wote hawapo na sasa amebakia Mkurugenzi ambaye hawezi kujitoa kwamba sio sehemu ya kampuni na sheria inasema vizuri.

Amesema baada ya kwenda kuangalia hawakukuta mali zozote, hivyo alielekeza kwa sababu mwekezaji mkubwa wa kampuni hiyo hayupo ambaye ni raia wa Uingereza na Kenya, ameitaka Idara ya Uhamiaji kumzuia kutoka nje ya nchi Mkurugenzi wa kampuni hiyo aliyepo sasa, Bresing Kachambwa.

Pia NSSF wameiandikia barua Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kusaidia kupatikana jina kumleta nchini Mama Christin ambaye ndiye mwenye hisa nyingi kwenye kampuni hiyo.

Kwa mujibuwa Naibu Waziri huyo, ameielekeza Kurugenzi ya Idara ya Sheria ya NSSF kuandaa taratibu ya kumpeleka Kachambwa katika utaratibu wa mfungwa wa madai mpaka pale ambapo stahiki za wafanyakazi zitapatikana.

Mavunde alitoa raia kwa waajiri wote ambao wahajawasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa muda mrefu, kujisalimisha kwenye ofisi za NSSF kuanzia leo, vinginevyo watasakwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Amesema Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Menejimenti mpya ya NSSF ambayo katika kipindi cha muda mfupi imeongeza makusanyo kutoka sh. Bilioni 58 kwa mwezi mpaka kufikia zaidi ya sh. Bilioni 100 kwa mwezi.

“Menejimenti hii ya NSSF imefanyakazi kubwa kwa muda mfupi sana na imeonesha uzalendo wa kutosha kwenye kusimamia michango ya wafanyakazi na tunaweza kupiga hatua kubwa sana,” amesema.

Alisisitiza kuwa kuanzia sasa waajiri wote ambao wanakata michango ya wafanyakazi lakini hawaiwasilishi NSSF watasakwa popote walipo na kuchukuliwa hatua kali za kisheria, kwani Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli imedhamiria kumkomboa mfanyakazi.

Mavunde amesema Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Ofisi ya Kamishna wa Kazina NSSF watafanyakazi kwa pamoja kuhakikisha hakuna mfanyakazi yoyote atakayepata changamoto ya kutopata stahiki zake.

“Naagiza kuanzia leo (jana) waajiri wote ambao wanajua kabisa kwamba kuna michango ya wafanyakazi haijawasilishwa NSSF ni bora wajisalimishe mapema mbele ya Shirika kwa sababu hatua zitakazochukuliwa sasa ni kuwakamata waajiri hao ili wafanyakazi wapate stahiki zao kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Kwa upande wake, Kamishna wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Francis Mbindi,amewaelekeza maofisa kazi wote nchini kuhakikisha waajiri wote wanatekeleza na kuzingatia sheria za kazi.