Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online,Kigoma
Naibu Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Exaud Kigahe (Mb) amemuhakikishia muwekezaji wa kiwanda cha TROLLE MEES LE TANZANIA IVS LTD soko la uhakika la mafuta ya mawese baada ya kuanza utekelezaji wa kutatua changamoto zilizojitokeza kwenye ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Kigahe ameyasema hayo mkoani Kigoma wakati wa kupokea taarifa ya kamati ya kufanya tathimini ya changamaoto zilizojitokeza katika kuongeza thamani ya zao la mchikichi mkoani hapo,ambapo amesema muwekezaji huyo asiwe na wasiwasi kwani soko la uhakika la mafuta hayo lipo.
Akiwa mkoani Kigoma Februari 27 ,2023 Waziri Mkuu alipokea changamoto anuai kutoka kwa muwekezaji wa kiwanda cha kuchakata na kuongeza thamani mafuta ya mawese cha TROLLE MEES LE TANZANIA IVS LTD kinachomilikiwa na Abdalah Mwilima.
Aidha changamoto zilizoainishwa na muwekezaji huyo ni pamoja na upungufu wa malighafi ya zao la mchikichi, serikali impatie eneo la kupanda zao la mchikichi ili kuwa na malighafi ya kutosha ,
Vilevile umeme uliopo eneo la kiwanda kutokuwa na nguvu (low power) ya kutosha kuendesha mitambo iliyofungwa kiwandani hapo, hivyo kuomba Tanesco Mkoa wa Kigoma kufunga Transformer kubwa eneo la mradi.
Pia changamoto nyingine ilikuwa ni kutopata kiasi chote cha mkopo alichoomba katika benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) hivyo kuomba serikali imsaidie kupata mkopo huo kwa wakati.
Kutokana na changamoto hizo,Waziri Mkuu aliagiza Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara kupitia taasisi zake ikiwemo SIDO kushughulikia changamoto zote zilizoanishwa na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati.
Hivyo kutokana na maelekezo hayo Wizara iliunda kamati ya kushughulikia changamoto hizo kupitia taasisi zinazohusika na mnyororo wa uchakataji wa zao la mchikichi kuanzia hatua ya awali ya uchakataji hadi kumfikia mlaji ambapo taasisi zilizohusika katika kamati hiyo ni SIDO,WMA,TEMDO, CAMARTEC,TIRDO na TBS.
Akizungumza wakati wa kupokea taarifa ya kamati hiyo Kigahe amemuhakikishia mwekezaji huyo kuwa Wizara imepokea changamoto zote zilizoanishwa na kuzifanyia kazi kwa haraka sana huku baadhi zikiwa zimepatiwa ufumbuzi tayari na zingine zikiwa bado kufanyiwa kazi.
“Nikuhakikishie kuwa changamoto zote tumeanza kuzifanyia kazi baada ya kupokea maelekezo ya Waziri Mkuu,Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imeshafanyia kazi changamoto yako ya mambo ya kifedha limekamilika ,kuhusu Tanessco tumeongea na Meneja wa shirika hilo Mkoa wa Kigoma changamoto hiyo inafanyiwa kazi kwa uharaka zaidi,”amesema Kigahe.
Awali akimkaribisha Naibu Waziri Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara Dkt. Hasil Abdallah amemhakikishia Naibu Waziri utekelezaji wa changamoto zilizoanishwa kwa kusema kuwa,yeye akiwa kama mtendaji mkuu wa Wizara atahakikisha zao la mchikichi linawakwamua wananchi wa Mkoa wa Kigoma kwa kuwa ndilo zao la kimkakati katika mkoa huo.
“Tunataka viwanda vyetu vitumie mafuta ghafi kutoka katika viwanda vyetu kikewemo kiwanda hiki cha TROLLE MEES LE TANZANIA IVS LTD, tunataka wakulima wanaozalisha mchikichi kutoka Mkoa wa Kigoma wawe na uhakika wa kuzalisha zaidi, sababu soko litakuwepo la uhakika lakini hata mzalishaji atakuwa na uhakika wa kuzalisha zaidi maana atakuwa na uhakika ya malighafi,”amesema Dkt.Hashill.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato