March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yakamilisha ukarabati kivuko cha Mv. Kazi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

SERIKALI imesema imefanikiwa imekamilisha ukarabati wa kivuko cha MV Kazi, uliolihusisha kubadilishwa kwa injini pamoja na mifumo ya umeme na uendeshaji wa chombo hicho.

Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Mosses Mabamba, alisema ukarabati wa kivuko hicho umechukua siku nne na kugharimu jumla ya shilingi milioni 30.

“Baada ya kusimamisha kivuko hiki, tulilazimika kufanya matengenezo makubwa ikiwemo kubadilisha injini mbili mpya, kuboresha mifumo ya umeme pamoja na mifumo ya uendeshaji wa chombo hiki,”amesema Mabamba.

Amesema Serikali inatambua umuhimu wa huduma ya kivuko hicho hususan kwa wanafunzi na wananchi wanaotegemea usafiri huo, hivyo TEMESA kwa kushirikiana na Kampuni ya Azam wameandaa mpango wa muda kuhakikisha huduma zinaendelea wakati majaribio ya kivuko cha MV Kazi yakikamilishwa.

“Tunafahamu kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaoanza masomo, hivyo tumezungumza na wenzetu wa Azam ambao wametusaidia kuvusha abiria wakati sisi tukiendelea na majaribio ya kivuko chetu,”ameongeza.

Ameeleza kuwa, kwa mujibu wa taratibu za kiufundi, ni lazima kivuko kifanyiwe majaribio baada ya marekebisho, ambapo majaribio hayo yalianza jana asubuhi na ilipofika saa nane mchana, kivuko cha MV Kazi kilianza kurejea rasmi kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo ya Feri, Kivukoni na Kigamboni.

“Kwa utaratibu wetu, majaribio ni hatua muhimu na baada ya kuyakamilisha, kivuko chetu kitarejea kutoa huduma kama kawaida,”amesema.

Aidha, Mabamba amebainisha kuwa kwa sasa kivuko cha MV Kazi kina uwezo wa kubeba abiria 200 kwa safari moja, hatua inayolenga kupunguza msongamano na kurejesha hali ya kawaida ya usafiri katika eneo hilo.

Katika hatua nyingine,amesema kwa mujibu wa mkataba wa ukarabati, kivuko cha MV Magogoni kinatarajiwa kurejea kutoa huduma mwezi Aprili mwaka huu, huku kivuko cha MV Kigamboni kikitarajiwa kurejea mwezi Oktoba baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa. Baada ya hapo, kivuko cha MV Kazi nacho kitapangiwa matengenezo makubwa ili kuimarisha zaidi huduma.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wanaotumia kivuko hicho wamesema kurejea kwa huduma ya MV Kazi ni faraja kubwa kwani kutarahisisha shughuli zao za kila siku ikiwemo kwenda kazini, shuleni na kufanya shughuli za kibiashara. Hata hivyo, wameitaka Serikali kuendelea kuboresha huduma za vivuko ili kuepusha adha zinazojirudia.