January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yakagua mkongo wa taifa wa mawasiliano bandari ya Mtwara

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Mtwara

NAIBU Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew amefanya ziara ya kukagua ufikishaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika bandari ya Mtwara uliofanywa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), upatikanaji wa mawasiliano ya simu katika eneo hilo pamoja na mifumo ya TEHAMA inayotumika bandarini hapo

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mhandisi Kundo Mathew (wa tatu kulia) alipotembelea bandari ya Mtwara kwa lengo la kukagua miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano uliofikishwa katika bandari hiyo kwa lengo la kuwezesha mawasiliano ya simu na intaneti yenye kasi kubwa na uwezo mkubwa Kulia ni Mbunge wa Mtwara Mjini Hassan Mtenga akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya. Wengine ni wafanyakazi wa bandari na baadhi wataalam aliombatana nao katika ziara hiyo

Katika ziara hiyo Mhandisi Kundo ameambatana na wataalam kutoka taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo ambazo ni Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Shirika la Posta Tanzania (TPC) pamoja na wenyeji wake ambao ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini Dunstan Kyobya na wabunge wa majimbo matatu yaliyopo katika Mkoa wa Mtwara ya kukagua ubora na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

“Nimefika hapa kujiridhisha uwepo wa nyaya za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika bandari ya Mtwara zitakazofanikisha upatikanaji wa intaneti yenye uwezo mkubwa na kasi kubwa ili shughuli zote zinazoendelea bandarini zisikwame kwasababu ya kukosekana kwa huduma ya intaneti” amesema Mhandisi Kundo.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew (wa pili kushoto) akimsikiliza Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara Nobert Kalimbu (kushoto) wengine kutoka kulia ni Mbunge wa Mtwara Mjini Mhe. Hassan Mtenga akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya wakati wa kukagua ufikishaji wa miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano bandarini hapo.

Aidha, pamoja na kukagua ufikishaji wa miundombinu ya Mkongo wa Taifa katika bandari hiyo pia ametumia muda huo kukagua mifumo ya TEHAMA inayotumika kwenye bandari hiyo kama inafanya kazi na kusomana na kutoruhusu mianya ya upotevu wa mapato na kukagua upatikanaji wa mawasiliano ya simu katika eneo la bandari hiyo

Katika hatua nyingine Mhandisi Kundo amezungumzia mwingiliano wa mawasiliano ya simu na nchi jirani ya Msumbiji yaliyolalamikiwa na wabunge na kutolea ufafanuzi kuwa mwingiliano wa mawasiliano katika maeneo ya mipakani yanasababishwa na uwezo wa minara ya mawasiliano iliyopo eneo husika pamoja na ramani ya mipaka ya kijiografia ya eneo husika inavyoingia na kutoka hivyo kusababisha eneo lenye mtandao wenye nguvu zaidi ndio utakaopatikana

Ameongeza kuwa Wizara hiyo ipo katika hatua za kuhakikisha minara inayojengwa kuanzia sasa inakuwa na uwezo wa 3G na kuendelea pamoja na kuiboresha minara ya zamani iliyokuwa na uwezo wa 2G kwenda 3G na kuendelea ili kuhakikisha kunakuwa na mitandao yenye nguvu itakayowezesha kupatikana kwa huduma ya mawasiliano ya simu na intaneti

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew akizungumza katika kikao cha ndani katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara kabla ya kuanza ziara yake wilayani humo ambapo alitembelea bandari ya Mtwara kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano uliofikishwa bandarini hapo pamoja na kutembelea baadhi ya maeneo yenye changamoto ya mawasiliano ya simu katika kata ya Mitengo

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wabunge wa majimbo matatu ya Mtwara Mjini Abdallah Chikota (Mb) Nanyamba,Hassan Mtenga (Mb) Mtwara Mjini na Issa Mchungaela (Mb) Lulindi, mbali na kuzungumzia mahitaji ya huduma za mawasiliano katika maeneo yao kwa niaba ya wananchi pia wametumia fursa hiyo kumshukuru Mhandisi Kundo kwa kufanya ziara hiyo na kuahidi kuendelea kushirikiana ili kutatua changamoto za mawasiliano zilizopo katika Mkoa huo.