March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yajipanga kutumia teknolojia ya AI

Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dar

SERIKALI imesema imejipanga kikamilifu kutumia teknolojia ya Akili Mnemba (AI) ili kuongeza ufanisi, kasi na ubora wa utoaji huduma kwa wananchi na kuhakikisha wanapata huduma kwa wakati.

Hayo yamebainishwa jijini Dar-es-Salaam na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Daudi, wakati akifungua mdahalo kuhusu matumizi ya Akili Mnemba katika kuboresha huduma kwa umma ulioandaliwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC).

Daudi amesema pamoja na Serikali kuendelea kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika miaka ya hivi karibuni, ukuaji wa kasi wa teknolojia ya Akili Mnemba umeleta mazingira mapya yenye changamoto na fursa katika utumishi wa umma, hivyo kuna ulazima wa kuendana na mabadiliko hayo.

“Ni dhahiri kuwa mabadiliko ni makubwa katika mazingira na kasi ya ukuaji wa teknolojia. Hatuwezi kubaki nyuma wakati dunia inakwenda kwa kasi. Nasi serikalini tunapaswa kutumia teknolojia ya akili mnemba kuhakikisha wananchi wanafaidika na huduma zinazotolewa kwa haraka na kwa ufanisi zaidi,” amesema Daudi.

Ameeleza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yataisaidia Serikali kupata majawabu sahihi kwa wakati, kutatua changamoto za wananchi kwa ufanisi na kuwafikia kwa wakati muafaka.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali tayari imeanza kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kwa kutumia teknolojia za kisasa, akitolea mfano eneo la ajira ambapo mifumo ya kidijitali imeanza kutumika kuboresha mchakato huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dk. Ernest Mabonesho, amesema matumizi ya Akili Mnemba katika utumishi wa umma ni hatua muhimu itakayorahisisha utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi kwa watumishi.

“Kazi yetu kubwa ni kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma hasa katika mambo mapya yanayoibuka. Utumishi wa umma unabadilika,” amesema Dk. Mabonesho.

Amebainisha kuwa ingawa Akili Mnemba ni dhana mpya katika utumishi wa umma, ni teknolojia isiyoweza kuepukika kutokana na mchango wake katika kuongeza wepesi wa utoaji huduma, uwazi na ufanisi.

Naye mshiriki wa mdahalo huo, Mahyolo Kalokola, amesema mjadala huo umemfungua macho kuhusu fursa zilizopo katika matumizi ya teknolojia ya Akili Mnemba na umuhimu wake katika kuboresha utendaji kazi serikalini.