May 30, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yajipanga kudhibiti matumizi yasiyo sahihi kuelekea uchaguzi mkuu

Na Heri Shaaban,Timesmajiraonline,Dar es Salaam

SERIKALI imesema imejipanga kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya mitandao kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Hayo yasemwa jijini hapa leo,Mei 29,2025  na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi, wakati wa kikao cha maandalizi kuelekea ufunguzi wa mkutano wa Jukwaa la Afrika kuhusu masuala ya utawala wa mtandao unaotarajiwa kufunguliwa rasmi Leo jijini Dar es Salaam.

Amesema wakati wa chaguzi mbalimbali baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vibaya mitandao hasa kudhalilisha wanawake na kuonya kuwa hawatavumiliwa kwani sheria itafuata mkondo wake.

“Wanawake tumekuwa tukidhalilishwa hasa nyakati kama hizi tunapoelekea kwenye chaguzi lakini sisi kama Serikali tuko imara kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 tumejipanga vizuri, tutadhibiti wale wote ambao watatumia vibaya mitandao sheria itafuata mkondo wake, hivyo niwasihi sana hasa vijana watumie vizuri mitandao,”amesema Mahundi.

Amesema pia wanaendelea kuuenga video vya kukuza bunifu ambavyo vinaendelezwa na Time ya Tehama nchini na kwamba vituo vinane vinaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Amesema katika mkutano huo watajadili kwa upana masuala ya intaneti kwa mustakabali mzima wa taifa letu kwa kushirikiana na nchi nyingine za Afrika na kuhakikisha jamii inaendelea kupata uelewa wa masuala ya intaneti.

Naye Mkurugenzi wa Miundombinu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Leo Magomba,amesema fursa mbalimbali zinapatikana kupitia mtandao hivyo ni wajibu kuhakikisha wanatumia vema mitandao ili waweze kunufaika.

Jukwaa hilo linatarajia kuwaleta pamoja wadau zaidi ya 1,000 kutoka nchi mbalimbali za Afrika huku Tanzania ikipata heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo.