Na Mwandishi wetu Timesmajira online
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini makubaliano ya maridhiano na watoa huduma wa mawasiliano yenye thamani ya Shilingi bilioni 50 kama malipo ya matumizi ya miundombinu tangu kujengwa kwake.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Jijini Dar es salaam Waziri wa habari, mawasiliano na Teknolojia Nape Nnauye amesema makubaliano hayo yamelenga kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na kujumuisha Kampuni kubwa za simu za Aitel Tanzania, Honora Tanzania (Tigo) na Vodacom.
Amesema dhamira ya serikali ya awamu sita iliyopo chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wote .
Amesema ni muhimu kuendeleza sekta ya Teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT) Kwa ajili ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kujitolea kwake kukuza sekta ya mawasiliano “amesema Nnauye
Aliendelea kueleza kuwa makubaliano hayo yalianzishwa mnamo Octoba 4 mwaka 2011 na yalilenga kuimarisha miundombinu ya mawasiliano ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mtandao wa mkongo wa taifa katika maeneo ambayo ayakuwa na huduma ya mawasiliano.
“Serikali imedhamiria na inafikia lengo la kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia watanzania wote na kuongeza Kasi ya ukuaji wa uchumi wa kidigitali na kufikia asilimia 85 ya watanzania wenye ufikiaji wa infaneti ya Kasi ifikapo mwaka 2025” amesema Waziri Nnauye
Aidha aliwaomba watoa huduma za mawasiliano kuendelea kuwekeza katika miundombinu Ili kufikia wananchi wengi zaidi .
Pia Waziri Nnauye aliwapongeza viongozi wa Serikali walioshiriki katika majadiliano na hatimaye kifikia muafaka wa pande zote mbili.
Awali Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI na Mwenyekiti wa Timu ya Serikali ya Majadiliano Adolph Nduguru ameipongeza Timu nzima ya majadiliano kwa kufanya kazi kwa uzalendo jambo ambalo limesaidia kazi hiyo kukamilika kwa ufanisi na ueledi na hivyo kifikia muafaka jambo linalosaidia kufungua ukurasa Mpya wa mashirikiano
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Timu ya Wataalamu ya serikali Paul Kadushi ameishukuru serikali kwa kuwateua na kuiamini timu hiyo ambayo imeundwa na wataalamu wa aina mbalimbali kwa lengo la kutoa ushauri wa masuala muhimu.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba