Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima amesema licha ya kuendelea kwa vitendo vya ukeketaji nchini lakini bado Serikali haijaridhika na upunguaji huo ndio maana imeendelea kuweka mipango madhubuti ya kupambana na ukatili huo dhidi ya wanawake na Watoto wa kike ili kutokomeza kabisa.
Aidha dkt.Gwajima ametaja mikoa mitano ambayo ni vinara wa vitendo vya ukeketaji huku mkoa wa Manyara ukitajwa kuongoza kwa vitendo hivyo kwa asilimia 58.
Dkt.Gwajima ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku ya ukeketaji duniani ambayo huadhimishwa Februari 6 ya kila mwaka ametaja mikoa inayofuatia kuwa ni pamoja na Dodoma 47%, Arusha 41%, Mara 32% na Singida 31.
“Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti wa Afya na Demografia ya Watu Tanzania (TDHS 2015/2016), mmoja kati ya wanawake 10 wenye umri kati ya 15 – 49 wamekeketwa ambapo asilimia 35 ya wanawake hao walikeketwa kabla ya kufikisha mwaka mmoja. “Amesema Dkt.Gwajima huku akiongeza kuwa
“Kulingana na taarifa hizi, hali ya ukeketaji imekuwa inapungua kutoka 18% mwaka 1996 kufikia 15% mwaka 2010 na 10% mwaka 2015/2016…;upungua huku kunatokana na jitihada za serikali, asasi za kiraia na wadau wengine wanaoshiriki katika kutokomeza ukeketaji na kubadili mitizamo ya jamii kuhusu mwanamke na mtoto wa kike.”
Aidha amesema maadhimisho haya yanatoa fursa kwa Serikali na Wadau wa masuala ya ukeketaji kutathmini hatua iliyofikiwa katika kutekeleza afua za kutokomeza ukeketaji nchini.
Dkt.Gwajima amesema mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa afua hizo yanatoa fursa kwa wadau kukutana na kubadilishana uzoefu wa namna bora zaidi ya kukabiliana na vitendo vya ukeketaji unaofanywa na baadhi ya jamii zetu kwa kisingizio cha kudumisha mila.
Siku ya kimataifa ya kupinga vitendo vya Ukeketaji inaadhimoshwa kitaifa katika Mkoa wa Mara ambapo kaulimbiu ya maadhimisho hayo kitaifa ikiwa ni “Tuongeze Uwekezaji, Kutokomeza Ukeketaji”
Dkt.Gwajima amesema kaulimbiu hiyo inahimiza nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ikiwa pamoja na Tanzania kuongeza uwekezaji wa rasilimali za kutosha ili kutekeleza afua za kuzuia na kukabiliana na athari za ukeketaji ikiwa ni pamoja na kuwabaini na kuwasaidia wahanga wa ukeketaji katika jamii.
Aidha amesema, Ukeketaji ni mojawapo ya ukatili wa kijinsia dhidi ya mwanamke na ukiuka wa haki za wanawake na watoto wa kike,Kichocheo kikuu cha vitendo vya ukeketaji ni mila na desturi za baadhi ya makabila katika jamii ambapo jamii inayokeketa huamini kuwa msichana aliyekeketwa anakuwa tayari kuolewa bila kujali umri wake.
“Mtazamo huu umepelekea kuongezeka kwa mimba na ndoa za utotoni pamoja na madhara mengine ya kiafya na kisaikolojia ambapo madhara makubwa kwa wanawake na watoto wa kike ni athari za kisaikolojia kama msongo wa mawazo kwani vitendo hivyo hufanywa bila ridhaa ya wahusika.”amesema na kuongeza kuwa
“Madhara ya kiafya kama maumivu makali, kutokwa damu nyingi, kuuguza kidonda, changamoto za kujifungua na uwezekano wa kupoteza maisha maambukizi ya magonjwa ya ngono, pamoja na maambukizi ya kujirudia kwenye njia ya uzazi na njia ya mkojo (UTI) na ukimwi”
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa