Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma
MBUNGE wa Viti Maalum, Dkt. Neema Majule, amehoji Serikali kuhusu hatua zilizochukuliwa kudhibiti mikopo hatarishi yenye riba kubwa inayotolewa na taasisi zisizo rasmi nchini.
Dkt. Majule aliuliza swali hilo Bungeni jijini Dodoma akitaka kufahamu mikakati ya Serikali katika kuwalinda wananchi dhidi ya mikopo hiyo inayowaumiza kiuchumi.
“Je, Serikali imechukua hatua gani kudhibiti mikopo hatarishi yenye riba kubwa inayotolewa na baadhi ya taasisi zisizo rasmi?” alihoji Dkt. Majule.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, alisema Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imechukua hatua kadhaa kudhibiti mikopo hiyo.
Alisema hatua hizo ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kwamba utoaji wa mikopo unapaswa kufanywa na watoa huduma wenye leseni kutoka BoT, kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 pamoja na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018.
Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa Serikali imewatambua na kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya watoa mikopo wasioidhinishwa, ambapo jumla ya programu 69 za mikopo ya kidigitali zilizokuwa zikitoa mikopo bila leseni zilisitishwa, huku programu nyingine 126 zikifungiwa.
“Pia Serikali imetoa mwongozo maalum kwa watoa huduma za mikopo ya kidigitali ili kuhakikisha uwazi, uendeshaji wa kimaadili, utoaji wa taarifa kamili kuhusu gharama za mikopo pamoja na ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha,” alisema.
Alibainisha kuwa Serikali imeandaa rasimu ya kanuni za kusimamia mikopo ya kidigitali, ambazo zinatarajiwa kuanza kutumika mwaka wa fedha 2026/2027, kwa lengo la kuimarisha udhibiti wa wakopeshaji wa kidigitali nchini.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama