Na Zena Mohamed,Timesmajira Online, Dodoma
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema serikali imeazimia kuendeleza utekelezaji wa mkakati wa kutokomeza ukatili na mauaji ya wazee nchini.
Hayo yamesemwa jijini hapa jana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mwanaid Khamis wakati akisoma hotuba ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee.
Amesema katika kutimiza azma ya kuendelea kuwalinda wazee pamoja na kuimarisha huduma nyingine, serikali ipo katika hatua za mapitio ya sera ya taifa ya wazee ya 2003, ambayo inaweka msisitizo kwenye kuimarisha upatikanaji wa haki ya ulinzi na usalama kwa wazee.
Mwanaid amesema sera inayofanyiwa mapitio, inalenga kuimarisha mifumo ya ulinzi shirikishi katika jamii ya kuwalinda wazee kutokana na hatari ya kufanyiwa vitendo vya ukatili, pamoja na mifumo ya upelelezi na uendeshaji wa mashauri ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wazee.
“Kutokana na ukweli kwamba hali duni ya kipato ni miongoni mwa sababu zinazochangia vitendo vya ukatili kwa wazee, serikali inalenga kuhakikisha wazee wanawezeshwa katika kubuni na kuendesha shughuli za ujasiriamali kupitia vikundi vidogo vidogo kwenye jamii, ili kuwawezesha kuinua kipato na kumudu mahitaji yao ya msingi,” amesema.
Pia amesema, wazee watawezeshwa kushiriki katika shughuli za michezo na burudani ili kuimarisha afya zao na kuwajenga kisaikolojia.
Amesema katika jitihada hizo za kuimarisha ulinzi kwa wazee, serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea na mapambano ya kutokomeza vitendo vya ukatili na mauaji ya wazee kwa kuongeza msukumo na kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kutokomeza mauaji ya wazee kwa kipindi cha miaka mitano (2018/19-22/23).
Pamoja na hayo, amesema kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau, vitendo vya ukatili na mauaji ya wazee nchini vimedhibitiwa kwa kiasi kikubwa.
“Kwa mujibu wa taarifa kutoka Jeshi la Polisi, mauaji ya wazee yamepungua kwa kiwango kikubwa kutoka 577 mwaka 2014 hadi wazee 34 Desemba 2020,” amesema.
Hata hivyo alisema, serikali inadhamiria kuongeza jitihada na kuhakikisha mauaji ya wazee yanakwisha kabisa.
“Serikali katika mapitio ya sera ya wazee ya mwaka 2003, imezingatia kuweka msisitizo zaidi katika kuhakikisha wazee wanapata huduma ya msaada wa kisaikolojia na ushauri nasaha ili kusaidia kuimarisha afya na ustawi wao,” amesema.
Amesema kwa mujibu wa mwongozo wa kitaifa wa utoaji wa huduma za msaada wa kisaikolojia wa mwaka 2021, matatizo mengi ya kiafya na kimahusiano yanayowakabili wazee yanatibika kikamilifu kupitia msaada wa kisaikolojia na ushauri nasaha.
Pia amesema kupitia mpango wa serikali wa kuboresha huduma za afya, imeendelea kuhakikisha kuwa kila kituo cha afya cha na hospitali zinakuwa na madirisha maalumu kwa ajili ya matibabu kwa wazee.
“Mpaka sasa kuna jumla ya madirisha 2,335 mahususi kwa ajili ya kutolea huduma za matibabu kwa wazee,” amesema.
Kutokana na hayo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora(THBUB) imesema kunahitajika kuwekwa kwa mifumo madhubuti ya kulinda na kutetea haki za makundi maalumu yanayohitaji ulinzi wa jamii husika.
Akitoa salamu za tume hiyo Kamishna wa THBUB, Dkt. Fatma Khalfan kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu katika maadhimisho hayo amesema katika kutekeleza suala hilo nchini,
Dkt. Khalfani ameongeza kuwa, heshima kwa wazee kwenye jamii nyingi za Kiafrika na Tanzania imekuwa ikipewa kipaumbele na mara zote, wazee wamekuwa sehemu ya familia.
Kutokana na umuhimu huo, alisema tume inawasihi wadau wote
kuenzi na kudumisha utamaduni huo kwa kutekeleza wajibu wao, ikiwemo kuwapatia wazee ulinzi na usalama, chakula, malazi na mavazi.
“Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002, Tanzania ilikuwa na wazee 1,952,041 (sawa na wanaume) 940,229 na wanawake 1,011,812) na katika sensa ya mwaka 2012 idadi ya wazee iliongezeka hadi kufikia 2,507,568(wanaume 1,200,210 na wanawake 1,307,358) sawa na asilimia 5.6 ya wananchi wote,” amesema.
Naye Meneja Programu wa haki na ushirikiano wa wadau kutoka Shirika la Help Age Intrnational Tanzania, Joseph Mbasha amesema shirika hilo ni miongoni mwa mashirika mtandao yaliyopigania utambulisho huo na lina dira ya kuona dunia ambayo kila mzee anaishi maisha yenye afya, hadhi na usalama.
Amesema katika kutekeleza azma hiyo, shirika hilo linatekeleza afua tano, ambazo ni kuboresha upatikanaji wa huduma za afya zilizo rafiki na bora kwa wazee.
Mbasha amesema afua nyingine ni kupinga vitendo vya ukatili na manyanyaso dhidi ya wazee, kutoa huduma jumuishi wakati wa majanga, kuhakikisha usalama wa kipato, pamoja na kuchagiza harakati za mabadiliko.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi